MAHUNDI: TUTAZIFANYIA KAZI CHANGAMOTO ZA UKOSEFU WA MAWASILIANO YA UHAKIKA PEMBA











Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Pemba

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeahidi kuzifanyia kazi changamoto zote kuhusu miundombinu ya mawasiliano zilizobainishwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), visiwani Pemba.

Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa mtandao wa intaneti wenye kasi na mawasiliano ya simu yenye uhakika katika maeneo kadhaa ya visiwa hivyo.

Akijibu hoja za wananchi kuhusu changamoto hizo leo tarehe 22 Novemba, 2024, Mhandisi Mahundi aliyepo visiwani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya Mawasiliano, amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha huduma za mawasiliano zinamfikia kila Mtanzania, wakiwemo wa maeneo ya visiwa kama Pemba.

“Huduma za mawasiliano ni nyenzo muhimu ya maendeleo, tunalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata mawasiliano bora na ya uhakika, bila kujali eneo alipo,” amesema Naibu Waziri Mahundi.

Amesema atahakikisha anafuatilia kwa karibu changamoto zote zilizobainishwa na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa haraka, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha mawasiliano yanakuwa daraja la maendeleo kwa wananchi wote.

Awali Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Mwasalyanda, alielezea juhudi zinazofanywa na mfuko huo katika kusogeza huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini na visiwani, huku akiahidi kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano katika kushughulikia changamoto zilizoainishwa.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mahundi ameambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ofisi ya Zanzibar, Bi. Esuvatie-Aisa Masinga kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar.
Previous Post Next Post