Na Mapuli Kitina Misalaba
Bahati Kizimbani, anayekadiriwa kuwa na umri wa
miaka 45 na mkazi wa Mseki kata ya Bulungwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
mkoani Shinyanga, amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa mapanga sehemu
mbalimbali za mwili wake.
Kwa mujibu wa Diwani wa kata ya Bulungwa, Mhe.
Kalwani Mteganoni, amesema tukio hilo limetokea leo alfajiri wakati Kizimbani
akiwa njiani kuelekea shambani na mpwa wake kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Akisimulia tukio hilo, Diwani Mteganoni ameeleza
kuwa, "Watu wamelala salama lakini asubuhi tuliposikia mwano na kelele tulifuatilia na kukutana na mwili wa
Bahati ukiwa na majeraha mengi ya mapanga, wakati huo alikuwa amekwenda
shambani na mpwa wake, walipofika katikati ya njia ghafla wakaona watu wawili
wakiwa na makoti na tochi. Hawa watu walimvamia na kumkata mapanga sehemu
mbalimbali, ikiwemo kichwani na mkono ambao ulikatwa kabisa, na kusababisha
kifo chake."
Diwani Mteganoni ameendelea kueleza kuwa, mpwa
aliyekuwa pamoja na marehemu alikimbia baada ya tukio hilo na kwenda kuita
watu, lakini walipofika, washambuliaji walikuwa tayari wameondoka na hawakuweza
kutambulika.
"Sisi
kama viongozi wa kata, tumeshangazwa na tukio hili na tunaomba serikali kupitia
jeshi la polisi kuendeleza uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji haya na
kuwafikisha wahusika mbele ya sheria, Bahati alikuwa mtu wa kawaida aliyekuwa
akijihusisha na uganga wa jadi na kilimo, na kifo chake kimetupa hofu kubwa,
hasa wakati huu ambapo matukio ya mauaji yamekuwa yakiongezeka."
Mhe. Mteganoni pia amewaasa wananchi waendelee
kuchukua tahadhari kuhusu usalama wao, hasa wanapokuwa wanakwenda mashambani
asubuhi au usiku. "Ni muhimu kuwa na umakini na tahadhari zaidi, kwani hali
ya usalama imekuwa tete,"
Misalaba Media bado inaendelea kufuatilia taarifa
zaidi kutoka kwa mamlaka husika ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na
hatua zinazochukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi wa kata ya Bulungwa
na maeneo jirani.