Na Mapuli Kitina Misalaba
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, leo
Novemba 20, 2024, amezindua rasmi kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
wagombea wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Shinyanga.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024,
ukihusisha viongozi wa Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Wajumbe watakaohudumu hadi
mwaka 2029.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Bubiki, Wilayani
Kishapu, ambapo Bashe ametangaza kuwa CCM tayari imejihakikishia ushindi wa
asilimia 77.
Akizungumza katika tukio hilo, Bashe amesema Mkoa wa
Shinyanga una jumla ya Mitaa 90, Vijiji 506, na Vitongoji 2,703, huku wagombea
wa CCM wakishikilia nafasi kubwa zaidi ikilinganishwa na vyama vya upinzani
ambavyo vimeweka wagombea asilimia 23 pekee.
Bashe amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku
ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM, akisisitiza kuwa chama hicho
ndicho kinachoweza kuleta maendeleo ya kweli.
Bashe ameahidi kwamba kabla ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itahakikisha wakazi wa Bubiki
wanapata huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.
Aidha, amebainisha juhudi za kuboresha kilimo cha
pamba kwa kutoa mbegu na madawa bure kwa wakulima, pamoja na kuajiri maofisa
ugani 2,000 ili kila kijiji kipate mtaalam wa kilimo mwenye pikipiki kwa ajili
ya kuwahudumia wakulima.
Kwa upande wa bei ya pamba, Bashe amesema serikali
itaweka mfumo wa uwazi zaidi kwa kuonyesha bei katika kila AMCOS, na wakulima
watapewa risiti ili kupata malipo sahihi kulingana na bei ya siku husika.
Aidha, ameeleza kuwa uchunguzi unaendelea dhidi ya
mtandao wa watu walioiba mbegu za pamba katika kijiji cha Mwamishoni, Kata ya
Bubiki ambapo ameonya kuwa ginery zitakazobainika kununua mbegu hizo za wizi
zitafutiwa leseni zao za biashara.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mabala
Mlolwa, amesema chama hicho kimejipanga kushinda kwa kishindo ili kumpa zawadi
Rais Samia kwa maendeleo aliyoyaleta mkoani humo.
Mbunge wa Jimbo la
Kishapu Mhe. Boniphace Butondo, amesisitiza kuwa CCM itashinda kwa
kishindo, akitoa shukrani kwa Waziri Bashe kwa kuisaidia serikali kutoa
matrekta 24 kwa wakulima wa Kishapu, hatua inayopunguza gharama za kulima
kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 35,000 kwa ekari moja.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini
Mhe. Paschal Patrobas Katambi, amewahimiza wananchi kuwachagua wagombea wa CCM
pekee ili kuwepo na mnyororo wa uongozi thabiti unaoweza kuwaletea maendeleo.
Naye mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy
Mayenga ameendelea kuwasisitiza wananchi kuchangua viongozi wanaotokana na
chama cha mapinduzi ili kutatua haraka changamoto zilizopo ikiwemo changamoto
ya maji katika jimbo la Kishapu.
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,
awali akiwasili uwanjani kwa ajili ya ufunguzi wa kampeni za serikali za mitaa.
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,
akizungumza kwenye ufunguzi wa kampeni hizo.
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,
akizungumza kwenye ufunguzi wa kampeni hizo.