Na Mapuli Kitina Misalaba
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Shinyanga Mjini,
Mwalimu Alexius Kagunze, amejibu malalamiko ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kuhusu madai ya kuenguliwa kwa wagombea wao katika uchaguzi
wa serikali za mitaa.
Kagunze ameeleza kuwa baadhi ya wagombea
wameenguliwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni, na si kwa nia ya kuwanyima
nafasi.
"Hapo
wanaposema kwamba wagombea wameenguliwa, ni kwamba hawajakidhi vigezo, katika
sehemu nyingi wamepitishwa, lakini baadhi ya wagombea ambao hawajakidhi vigezo
wamekuwa wakikwepa kufuata hatua zote zinazotakiwa. Kwa mfano, unakuta mgombea
wa chama fulani amejaza fomu yake lakini sehemu inayotakiwa adhaminiwe yeye hajadhaminiwa
na mtu mwingine amejidhamini mwenyewe sasa hapo msimamizi atamteuaje kuwa
mgombea wakati yeye mwenyewe kajiharibia?”
"Au,
unakuta mgombea wa chama fulani ametakiwa kugombea ujumbe katika kundi fulani sasa
yeye ni wa kiume, lakini ameandika kwamba anagombea kuwakilisha kundi la akina
mama katika hali kama hii, msimamizi wa uchaguzi atamteuaje kuwa mgombea”.amesema
Kagunze
Kagunze pia ameeleza kwamba baadhi ya wagombea
hawajaandikishwa kwenye daftari la wakazi wa eneo wanalotaka kugombea, hali
ambayo inakiuka mojawapo ya masharti ya msingi.
"Mgombea
mwingine wa chama fulani unakuta anagombea lakini hajajiandikisha kwenye
daftari la wakazi, wakati moja ya sifa za mgombea ni kuwa mkazi wa eneo hilo sasa
huyo amejiengua mwenyewe, lakini lawama anazipeleka kwa msimamizi wakati
amejiondoa yeye mwenyewe,"amesema Kagunze
Kagunze amewataka wagombea kuendelea kutumia haki
zao za msingi kwa kufuata hatua zinazotolewa kisheria ili kuhakikisha mchakato
wa uchaguzi unakamilika kwa haki na uwazi.
"Baada
ya hapo, kama mgombea hajaridhika, anapaswa kuwasilisha pingamizi kwa msimamizi
wa ngazi ya kata Msimamizi atatafakari pingamizi aliloweka kama bado
hatoridhika, ataendelea na hatua inayofuata iwapo mgombea anaona ameonewa,
aende kwenye kamati ya rufaa inayoongozwa na katibu tawala wa wilaya, ambaye ndiye
mwenyekiti wa kamati hiyo. rufaa zimeanza leo na zitaendelea hadi tarehe 13,
ambapo watapata majibu yao hakuna anayekataliwa watumie haki zao za kimsingi,”
amesema Kagunze.
CHADEMA KANDA YA SERENGETI YADAI WAGOMBEA WAKE KUENGULIWA BILA SABABU (MAJIMBO 24) SHINYANGA, SIMIYU NA MARA
CHADEMA wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo.
TAZAMA VIDEO CHADEMA WANAONGEA