Na Mapuli Kitina Misalaba
Imeelezwa kuwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka
mitano amefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati wa mvua iliyonyesha leo
jioni Novemba 16, 2024 katika kijiji cha Seseko kata ya Mwamalili Halmashauri ya Manispaa ya
Shinyanga.
Tukio hilo limetokea majira ya saa kumi na mbili
jioni, wakati mtoto huyo alikuwa ameenda kucheza kwa jirani.
Akizungumza na Misalaba Media, Diwani wa kata ya
Mwamalili, Mhe. James Mdimi (Matinde), amekili kupotea taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa
mtoto huyo, aliyefahamika kwa jina la Delila Jisenza, alikumbwa na radi wakati
akiwa ndani ya jiko la kupikia chakula pamoja na watoto wengine.
“Ni
kweli tukio limetokea katika kata ya Mwamalili kijiji cha Seseko, kwa ndugu
Jisenza Maliseli, kwa taarifa za familia wanasema muda wa saa kumi na mbili
mtoto huyo alikuwa ameenda kucheza kwa jirani. Mvua ilianza kunyesha muda huo,
na watoto walikuwa ndani ya jiko, yaani nyumba ya kupikia chakula, baadaye radi
ilianguka na kusababisha tukio hilo, baba wa familia alipokuwa karibu na mtoto
wakati radi inaanguka, muungurumo wake ulimfanya azimie,”
amesema Diwani Matinde.
Mhe. Matinde ameongeza kuwa mwili wa marehemu kwa
sasa uko nyumbani kwa baba yake mzazi, na mtoto huyo alijeruhiwa kifuani pamoja
na upande wa mkono wa kushoto kutokana na tukio hilo.
Katika ushauri wake, Diwani amewataka wazazi na
walezi kuhakikisha watoto wanakuwa salama nyumbani mara wanapogundua dalili za
mvua.
“Ushauri wangu kwa wananchi, hasa wazazi na
walezi, ni kwamba wanapoona dalili za mvua wahakikishe watoto wanarudi nyumbani
pia, wachukue tahadhari kuwaweka katika maeneo salama zaidi,”
amesema Diwani Matinde.