Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Said Sakala, katikati akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 2, 2024.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Said Sakala, ameonesha furaha na matumaini makubwa katika siku yake ya kwanza rasmi kuongoza kikao cha kamati ya utekelezaji ya UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Sakala ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya
vijana katika mchakato wa kisiasa, akiwapongeza kwa kujitokeza kujiandikisha
kwenye daftari la wakazi na pia kushiriki kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
katika ngazi za serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji.
“Leo
nimefarijika sana siku yangu ya kwanza kuingia na kufanya kikao cha kawaida cha
kamati ya utekelezaji UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini,”
Ameendelea kwa kuwapongeza vijana wenzake
waliothubutu kugombea nafasi hizo na wale waliopitishwa kugombea huku akisisitiza
kuwa ujasiri huo ni ishara ya mabadiliko na kuonesha kuwa vijana wana ari ya
kuleta maendeleo katika jamii yao.
“Nipende
kuwapongeza vijana wenzangu kwa uthubutu huo na wale walioteuliwa kugombea
nafasi hizi za wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji,”.amesema
Sakala
Aidha, Sakala amewahamasisha vijana wote ambao
wamejiandikisha kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye kampeni kwa njia ya
amani na ustaarabu.
“Nitumia
nafasi hii kuendelea kuwahamasisha vijana wote ambao tumejiandikisha twende
tukafanye kampeni za ustarabu lakini pia tujitokeze kwa wingi kwenda kupigia
kura wenyeviti wetu wa mitaa wanaotokana na chama chetu cha Mapinduzi,”
amesema Sakala.
Katika upande wa maendeleo ya kiuchumi kwa vijana,
Sakala ameonyesha kufurahishwa na hatua za serikali kuanzisha utaratibu mpya wa
utoaji wa mikopo ya asilimia nne kwa vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga.
Amesema mikopo hiyo ni fursa kubwa kwa vijana wengi
ambao hawana ajira, na ametoa wito kwa vijana wa Shinyanga Mjini kujitokeza kwa
wingi kuomba mikopo hiyo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Sakala pia ameeleza maboresho yaliyofanywa katika
utoaji wa mikopo hiyo, ikiwemo kuongeza umri wa wanaostahili kuomba kutoka
miaka 18 hadi 35 na sasa hadi miaka 45, jambo linalowapa nafasi vijana wengi
zaidi kupata mikopo hiyo.
“Mikopo hiyo kwa sasa imeboreshwa umri
umeongezeka hadi miaka 45, kwahiyo vijana wenye umri huu kuanzia miaka 18 hadi
45 hii ni fursa kubwa kwetu,” amesema Sakala.
Pia, amezungumzia mabadiliko ya utaratibu wa mikopo
kwa vijana, ambapo sasa vijana wanaweza kuomba mikopo kama mtu binafsi badala
ya vikundi.
“Zamani ilikuwa ni lazima kuomba vijana
kuanzia watano lakini kwa sasa imeboreshwa zaidi ni kwamba mtu binafsi anaweza
kuomba huo mkopo kwa ajili ya kuweza kujikwamua kimaisha,”
amesema Sakala.
Sakala amehitimisha kwa kuwahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuomba mikopo na kuzitumia fursa hizo kwa malengo ya kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya Shinyanga Mjini na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Said Sakala, akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 2, 2024.