OFISA UTUMISHI NA WENZAKE 11 KIZIMBANI KWA UHUJUMU UCHUMI

 
NA MWANDISHI WETU, MARA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Musoma, mkoani hapa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Veronica Mgendi,  imefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 32001/2024 ya Jamhuri dhidi ya Ofisa Utumishi wa Wilaya Nico Amanyisye  Kayange na wenzake 11.

Washtakiwa wanashtakiwa kwa makosa ya kuendesha Genge la Uhalifu kinyume na Aya 4(1) (a) ya Jedwali la Kwanza na Vifungu vya 57(1) na (60) (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa Sura 200 Mapitio ya 2019, Matumizi Mabaya ya mamlaka kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 Mapitio ya mwaka 2019 kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57 (1) na 60 (2) Cha Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 Marejeo ya 2019 na kosa la kuisababishia Mamlaka hasara ya kiasi cha Sh. 205,720,071/- kinyume na Aya ya 10 (1) ya Jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura 200 Marejeo ya mwaka 2019.

Washtakiwa tisa kati ya 12 walikuwa ni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo yupo Amos Jeremiah Kusaja (Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya), Nico Amanyisye Kayange (Ofisa Utumishi wa Wilaya),Mona Shomary Bitakwate ( Ofisa Utumishi), Sangi Makenge Ruge (Mwekahazina wa Wilaya), Emmanuel Simon Mboje (Mkuu wa Idara ya Manunuzi), Abbas Ndyamukama na Shaban Shissebe Ndalu (Mhasibu), Hesbone Pius Bature (Mhasibu Msaidizi) na Nuru Yahya Yunge (Mganga Mkuu wa Wilaya)

Washtakiwa wa tatu waliobaki ni wazabuni ambao ni Thomas Michael Kwęka, Gabriel Mugini Kenene na Mseti Masanchu Maswi.

Akisoma hati ya mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Restituta Kessy akishirikiana na Zena Kisesa Novemba 11,2024 amesema washtakiwa hao kwa tarehe tofauti kati ya Juni na Julai 2021 walitumia mamlaka yao vibaya kwa kutofuata taratibu za manunuzi na kufanya malipo kwa Wazabuni bila vifaa vya ujenzi kusambazwa katika mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, hivyo kuisababishia hasara Halmashauri hiyo kiasi cha Sh. 205,720,071/-

Washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo, na shauri liliahirishwa hadi Desemba 2, 2024 kwa ajili ya kuwasomea Washtakiwa Hoja za Awali.

Washtakiwa waliweza kutimiza masharti ya dhamana hivyo kuachiwa kwa dhamana.
Previous Post Next Post