Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexius Kagunze, ameeleza kukamilika kwa asilimia 100 kwa maandalizi yote uchaguzi wa Serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika hapo kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26, 2024, Kagunze ameeleza kuwa, hatua zote za maandalizi zimefanyika kwa ushirikiano wa karibu na wadau wote wa uchaguzi wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa na kwamba, jumla ya vituo 285 vitatumika katika zoezi la upigaji wa kura katika Manispaa ya Shinyanga.
Amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutumia haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka, huku akiwasisitiza kudumisha amani wakati wote wa zoezi la uchaguzi.
Kagunze amesema Jumla ya vyama 9 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo, huku akivitaja vyama vya CCM na CHADEMA kuwa ndiyo vyenye wagombea wengi zaidi ambapo vingine vilivyobaki vimesimamisha wagombea katika maeneo machache.
Taarifa hiyo ya Msimamizi wa uchaguzi inakuja huku chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kupitia Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi, kikilamikia kuongezwa kwa vituo vipya 122 bila chama hicho kushirikishwa mapema ili kuandaa mawakala, kinyume na orodha ya vituo 163 walivyopewa hapo awali.
Uchaguzi huo wa Serikali za mitaa ambao utawapa fursa wananchi wa Tanzania bara kuwachagua Wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji pamoja na wajumbe wao, utafanyika kesho Jumatano Novemba 27, 2024, ambapo vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 Asubuhi hadi saa 10:00 jioni.