Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Makolo, ametembelea Kituo cha Mathew Day Care kilichopo Maganzo na kutoa elimu ya ukatili kwa watoto na walezi.
Akizungumza na watoto pamoja na walimu wa kituo hicho, Makolo amesema elimu hiyo inalenga kuwasaidia watoto kutambua haki zao na jinsi ya kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili. Aidha, amewataka walezi na walimu kushirikiana kwa karibu kuhakikisha mazingira ya watoto yanakuwa salama.
“Ukatili ni changamoto kubwa katika jamii yetu, na elimu hii ni hatua ya kwanza ya kujenga kizazi kinachojitambua na kujilinda,” amesema Makolo.
Kwa upande wake, mwalimu mkuu wa kituo hicho, Elizabeth Mathew, amepongeza juhudi za SMAUJATA katika kupambana na ukatili na kuomba elimu zaidi iendelee kutolewa kwa jamii nzima ya Maganzo ili kuongeza uelewa.
Watoto walioshiriki katika mafunzo hayo walionyesha kufurahishwa na mafunzo waliyopokea, wakisema kuwa sasa wanajua hatua za kuchukua endapo watakumbana na vitendo vya ukatili.
Elimu hiyo ni sehemu ya kampeni ya SMAUJATA inayolenga kutokomeza ukatili katika wilaya ya Kishapu na maeneo mengine ya Tanzania kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii.