Wananchi katika halmashauri ya Mpimbwe Jimbo la Kavuu Mkoani Katavi wameipongeza timu ya utabibu wa magonjwa ya macho kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa katavi na hospitali ya wilaya ya Mpimbwe kwa kuendesha kliniki ya afya ya macho.
Wataalam hao wameendesha kliniki ya afya ya macho kwa majuma mawili katika hospitali ya wilaya ya Mpimbwe iliyopo Tupindo kuanzia tarehe 11 hadi 26 Novemba 2024 na kufanikiwa kutibu wagonjwa 403 huku kati yao wagonjwa 140 walikutwa na tatizo la mtoto wa jicho.
Akitoa thamini ya zoezi hilo mratibu wa afya ya macho mkoa wa Katavi Dkt. Salome Renatus amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na wagonjwa wengi waliojitokeza kupona kabisa huku huduma hiyo ikuhusisha upasuaji kwa baadhi ya wagojwa
"Watu wengi waliojitokeza wameweza kupona kabisa na kurudi katika hali ya kawaida wapo ambao tumewafanyia huduma ya upasuaji hii ni kutokana na macho yako kuhitaji matibabu ya kina" amesema Dkt. Salome
Aidha Dkt Salome amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda kwa kuwapa ushirikiano hasa kuwahamasisha wananchi kufika hospitalini hapo.
"Sambamba na hayo tunashukuru mchango wa mhe. mbunge kwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupitia mikutano yake ya kikazi hivyo imesaidia idadi ya wagojwa wengi kuja".
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Geophrey Pinda amesema kufanyika kwa huduma ni kuunga jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa kuboresha miundombinu ya afya.
"Namshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutusogezea huduma hizi karibu kwa hapo awali zilikuwa zinapatikana mbali" Amesema Mhe. Pinda
Naye Antony Lutonja ( 78) amesema kuwa amehangaika kwa miaka mitatu kutafta tiba ya macho ambapo hatimaye timu hii imempa matumaini mapya ya kupona kutokana ma huduma hiyo.
"Sijaona huduma kama hii kwingine yaaan nilale leo niamke naona kama wengine naona mambo yanafanyika hapa ni mambo mazuri mno". Amesema Antony Lutonja.
Ikumbukwe huduma hii ya macho ya afya ipo chini ya ufadhili wa African Blind help shirika la afya kutoka Ujerumani ambalo limewezesjha kliniki ya macho hospitalini hapo.