SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA FEDHA ZA UMMA ZIZINGATIWE-MAJALIWA






SERIKALI imewataka Maafisa Masuuli na Watendaji wote Serikalini wazingatie sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma ili kutimiza ndoto na malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Novemba 8, 2024) wakati akiahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma. Amesema lengo la Serikali ni kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji katika kusimamia na kudhibiti ipasavyo ukusanyaji wa mapato na matumizi.

Amesema kuwa katika vikao vya bunge la 12 vilipokea na kujadili kwa kina Taarifa za Kamati za Bunge ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 ulioishia tarehe 30 Juni, 2023.

Waziri Mkuu amesema taarifa hizo za Kamati zinazotokana na Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. “Ninalipongeza Bunge lako tukufu kwa kuchambua kwa kina hoja zote za ukaguzi zinazohusu matumizi ya fedha za umma. Pamoja na kutoa maazimio ambayo kimsingi ni maelekezo mahsusi kwa Serikali.”

Waziri Mkuu amesema hoja zote zimeainishwa kwa ajili ya utekelezaji. Hivyo basi, ninaziagiza Wizara zote kuandaa kwa wakati taarifa za utekelezaji wa Maazimio yote kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati za Bunge, na kuziwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu ili iweze kuwasilisha taarifa ya Serikali kwa Mheshimiwa Spika.

“…sote ni mashahidi kwamba, Serikali imeendelea kufanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi chini ya uongozi wa Ndugu Charles E. Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Vilevile, Serikali imeendelea kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na Bunge lako tukufu kupitia maazimio na hoja zilizotolewa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi wakati wa uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “Vilevile, nitoe rai kwa wananchi wote kama walivyojitokeza kwenye kujiandikisha vivyo hivyo wajitokeze siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2024 kupiga kura.”
Previous Post Next Post