SHINYANGA: MKURUGENZI WA MIFUMO NA MAWASILIANO WA TASAF, JAPHET BOAZ, AELEZA MAFANIKIO YA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI, RC MACHA ATOA WITO

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Japhet Boaz, amesema mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeleta mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake, ukilenga kuinua hali ya maisha ya Watanzania wenye kipato duni.

Amebainisha hayo leo, Alhamisi, Novemba 7, 2024 wakati akisoma taarifa yake kwenye kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kwa viongozi na waandishi wa habari ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

 Boaz ameeleza kuwa mpango huo, ulioanzishwa rasmi mwaka 2013, umefanikiwa kusaidia kaya maskini kwa kuwapatia msaada wa kifedha na kuwahusisha katika ajira za muda ili kujiongezea kipato.

Boaz amebainisha kuwa mpango wa TASAF unahudumia zaidi ya kaya milioni 1.37 katika Halmashauri 184 za Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

Amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2024, jumla ya Shilingi bilioni 945.5 zimetolewa kama ruzuku kwa kaya zilizoorodheshwa kwenye mpango huo, huku kaya zipatazo 534,606 zikipokea malipo kupitia njia za kielektroniki.

"Ajira za muda kwa walengwa ni sehemu muhimu ya mpango wetu, ambapo jumla ya miradi 27,863 imeibuliwa na wananchi wenyewe na kutekelezwa na walengwa wa mpango huu miradi hiyo imewezesha kuboresha miundombinu ya kijamii kama barabara, mabwawa ya kuhifadhi maji, na maeneo ya umwagiliaji," amesema Boaz.

Pia ameongeza kuwa TASAF imefanikisha kuwaondoa katika umaskini uliokithiri kaya zipatazo 394,500 zenye wastani wa watu milioni 1.8, ambazo sasa zimeweza kujitegemea na hivyo kuhitimu kutoka katika mpango wa msaada wa kifedha.

Wakati huo huo Boaz amesema waandishi wa habari ni wadau muhimu wa mpango huo, kwani wanahitajika kuelimisha umma kuhusu dhamira ya mpango na kuondoa dhana potofu zinazohusishwa na ajira za muda zinazotolewa kwa walengwa.

Aidha Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Japhet Boaz itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha jamii inaelewa malengo na mafanikio ya mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, ambao unatekelezwa kwa lengo la kujenga taifa lenye usawa wa kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha amewasihi waandishi wa habari kuandika kwa usahihi ili kuepusha upotoshaji ambao umekuwa ukiibuliwa na baadhi ya watu kuhusu walengwa wa TASAF kufanya kazi za muda.

Mhe. Macha amewasisitiza waandishi wa habari kutumia weledi wao kuelimisha umma kwa usahihi kuhusu mpango huo, huku akieleza kuwa TASAF inawasaidia walengwa kwa kuwapa ajira za muda kama sehemu ya kujiongezea kipato.

Amefafanua kuwa kazi hizo si adhabu, bali ni sehemu ya kujenga uwezo wa walengwa kujitegemea kiuchumi.

"Walengwa wa TASAF kufanya kazi za muda si adhabu mbali ni fursa ya kujiongezea kipato na kujenga ujuzi hata wafungwa wanaofanya kazi siyo adhabu yao, adhabu yao ni kutengwa na jamii,"

"Kuna dhana potofu kuwa walengwa wa TASAF wanafanyishwa kazi kama wafungwa, jambo ambalo halina ukweli ni muhimu sasa waandishi wa habari wapate elimu ili kuondoa upotoshaji huu,” amesema Macha.

Wakati huo huo RC Macha amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, ili kuchagua viongozi wenye nia ya kuleta maendeleo katika jamii.

Baadhi ya waandishi wa habari wamepongeza mafanikio ya mafunzo yaliyotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuhusu mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambapo wamesema kuwa wamejipatia uelewa wa kina kuhusu dhima ya TASAF katika kupunguza umaskini na kuwawezesha walengwa kupata msaada wa kifedha na ajira za muda kwa ajili ya kujiongezea kipato.

 Wamepongeza jitihada za Serikali kupitia TASAF katika kuhakikisha kaya maskini zinapata msaada unaohitajika, huku wakiahidi kuandika habari kwa usahihi ili kuepuka upotoshaji wa taarifa.

Wamesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuboresha taarifa zinazohusiana na mpango wa TASAF, na kwamba wataendelea kushirikiana na vyombo vya Serikali ili jamii iweze kupata taarifa sahihi na za kuaminika kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na umaskini.

Kikao hicho cha siku mbili kimeratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kwa lengo la kuongeza uelewa wa utekelezaji wa mpango huo kwa jamii.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria kikao hicho wakiwemo Wenyeviti wa Klabu za Waandishi kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Tabora, Geita, na Simiyu, wakiwa na dhamira ya kupata uelewa wa kina kuhusu mpango huo ambao unalenga kuinua maisha ya kaya maskini kwa msaada wa kifedha na ushauri wa kiuchumi.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zimefundishwa ikiwemo utekelezaji wa shughuli za TASAF na mpango wa kunusuru kaya maskini (Miradi ya jamii na mifumo ya utekelezaji) pamoja na ushirikiano wa TASAF na vyombo vya habari huku majadiliano mbalimbali yakifanyika.

Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Japhet Boaz, akisoma taarifa yake kwenye kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kwa viongozi na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha awali akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kwa viongozi na waandishi wa habari.

Mratibu wa TASAF Mkoa wa Shinyanga Maligisa James Dotto akizungumza kwenye kikao hicho.

Picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja

 

TAZAMA VIDEO

Previous Post Next Post