SHINYANGA: MONGELLA AWASISITIZA WANANCHI KUPIGIA KURA CCM KESHO

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mhe. John Mongella, akizungumza kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika Mkoa wa Shinyanga leo Novemba 26, 2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mhe. John Mongella, amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kesho, Jumatano Novemba 27, 2024, kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji na wajumbe wake huku akiwaomba kuchagua viongozi wa CCM.

Mongella ametoa wito huo wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi huo uliofanyika katika kata ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, akibainisha kuwa vitongoji, vijiji na mitaa ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

"Tunapozungumzia msingi wa maendeleo ni kitongoji, kijiji ni mtaa. Bila kuimarisha msingi, nyumba haiwezi kusimama. Myambue kuwa vitongoji, vijiji na mitaa ndiyo msingi wa maendeleo," amesema Mongella.

Amewahimiza wananchi kutumia haki yao ya kupiga kura kwa busara ili kuendeleza amani, mshikamano na maendeleo ambayo yamejengwa na serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"WanaShinyanga, leo tunapoenda kulala, kila mtu kwa imani yake amuombe Mwenyezi Mungu kesho afanye maamuzi ya hekima na busara. Mmeona tokea awamu ya kwanza hadi ya sita, nchi yetu imeendelea kuwa ya amani na mshikamano," amesema Mongella.

Kwa upande wa Mkoa wa Shinyanga, Mongella amesema kuna mitaa 90, vijiji 506, na vitongoji 2,703 ambapo ameeleza kuwa tayari CCM imepita bila kupingwa katika mitaa minne lakini amesisitiza kuwa ni muhimu kuwapa wagombea wa CCM kura za ndiyo.

"Nawaomba kesho watu tuamke asubuhi sana twende kwenye vituo vya kupigia kura. Vituo vitafungwa saa kumi jioni, wanaCCM tuwe wa kwanza. Lakini tafadhali hakikisha kesho hakuna mtu anayevaa mavazi yenye alama ya chama au kushika bendera, kwani sheria inazuia," amesisitiza Mongella.

Aidha amewakumbusha wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji na wajumbe kuwa ushindi wao utapaswa kutafsiriwa katika kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha maendeleo na ustawi wa kiuchumi.

Wananchi wa Shinyanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi kesho ili kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mhe. John Mongella, akizungumza kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika Mkoa wa Shinyanga leo Novemba 26, 2024.





Previous Post Next Post