Na Mapuli Kitina Misalaba
Farida Hamis William, mkazi wa kata ya Ndala katika
Manispaa ya Shinyanga, ni mfano wa mafanikio yanayotokana na mpango wa TASAF
ambapo kabla ya kujiunga na mpango huo, maisha yake yalikuwa na changamoto
nyingi ambapo kwa sasa ameeleza kuwa anajitegemea kiuchumi.
Leo Novemba 8, 2024 amezungumza na waandishi wa
habari akieleza kuwa aliishi katika mtaa wa Banduka, akiishi kwenye nyumba ya
tope ambayo alipewa bure na jirani mmoja baada ya kushindwa kumudu kodi.
"Kabla
sijajiunga na TASAF, nilikuwa na maisha magumu sana nilikosa hata mahali pa
kuishi na sikuwa na kipato cha uhakika," anasema Farida.
Amesema jina lake lilipendekezwa kwenye mkutano wa
hadhara ambapo baada ya kujiandikisha, Farida alianza kufanya kazi mbalimbali
zilizokuwa sehemu ya mpango wa TASAF, ikiwemo kazi za ujenzi na uchimbaji
barabara kuelekea Hospitali ya Mkoa ya Shinyanga kutoka Ndala hadi Mwawaza.
Ameeleza kuwa malipo ya kwanza aliyopokea kupitia
mpango huo yalikuwa ni shilingi elfu arobaini na nane, fedha ambazo alizitumia
kununua bata wawili, jike na dume.
"Baadaye
tuliendelea kufanya kazi za TASAF na hatimaye tukaanza kupokea fedha malipo
yangu ya kwanza yalikuwa shilingi elfu 48, ambapo nilinunua bata wawili, mmoja
jike na mwingine dume nilianza kuwafuga, na baada ya muda walizaliana bata huyo
alizaa watoto 12 kwa mara ya kwanza, na niliendelea na ufugaji huo hadi nikawa
na bata 90."amesema Farida.
Kwa msaada wa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Farida aliweza
kugharamia mahitaji ya familia yake, ikiwemo kuwasomesha watoto wake shuleni na
kwamba baada ya mtoto wake wa kiume kufaulu kidato cha nne na kupata nafasi ya kuendelea
na masomo ya juu jijini Dodoma, Farida
aliuza sehemu ya bata wake ili kugharamia ada na mahitaji mengine ya masomo.
"Nilipokuwa
nikiendelea na ufugaji wa bata, bado nilikuwa kwenye mpango wa TASAF, Fedha
nilizopata ziliisaidia familia yangu, ikiwemo kuwasomesha watoto wangu na
kununua chakula mtoto wangu wa kiume alipomaliza kidato cha nne, alifaulu
kwenda kusoma Dodoma niliuza baadhi ya bata na kubakiza watatu tu, na kwa fedha
niliyopata nikamlipia ada hadi akamaliza chuo."amesema Farida
Mpango wa TASAF pia ulimsaidia Farida kuboresha
makazi yake kwa hatua zaidi kwa pesa za TASAF na faida ya biashara zake,
aliweza kununua pumba junia 70 na kuzichoma tofali za kujenga nyumba alinunua
mabati na kujenga nyumba yake kwa ubora wa hali ya juu, hadi kufikia kuweka
sakafu nzuri chini, jambo ambalo lilikuwa ni ndoto kwake hapo awali.
"Pia
nilikuwa na mtaji wa kuuza matunda kupitia fedha za TASAF. Nilikuwa napokea
fedha na kuongeza kwenye biashara yangu ya matunda. Wakati nikiendelea na
biashara hizo, nilianza kununua mabati kidogo kidogo nilianza na bando mbili na
nusu, na baadaye nikaongeza mifuko ya saruji, hatimaye nikaweza kujenga nyumba
yangu ndogo ya sura ya suropu."amesema Farida
Farida anawashukuru sana watu wa TASAF, akisema kuwa
msaada waliompatia umebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa huku akimshukuru pia Rais Samia kwa kuanzisha
mpango huo ambao umemkomboa.
"Ningekuwa na changamoto nyingi kama TASAF
isingekuwepo kwa sababu mafanikio ya watoto wangu na biashara zangu yote yametokana
na TASAF," amesema Farida.
Malengo ya Farida sasa ni kuendelea kufuga bata
kwani biashara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwake ingawa kwa sasa ametolewa
kwenye mfumo wa TASAF, anaendelea kujitegemea kupitia biashara yake ya bata na
matunda.
"Malengo
yangu ni kuendelea kufuga bata kwa sababu wanakuwa msaada ninapopata shida;
nimeshapata wateja hapa hapa hivi sasa tumeondolewa kwenye mfumo wa TASAF,
lakini nashukuru sana kwa sababu sina shida, Bata hawa wamekuwa mtaji wangu
baada ya TASAF."
"Nashukuru mno TASAF kwa kuniwezesha, hapo awali sikuwa na wazo kwamba nitaweza kufuga bata, kufanya biashara, na hata kujenga nyumba yangu lakini nashukuru, nimefanikiwa, naishukuru serikali na pia namshukuru mama Samia kwa kutuona sisi."amesema Farida
Baadhi ya waandishi wa habari wakielekea katika familia ya Farida Hamis.