SHIRIKA LA YAWE NA RESTLESS DEVELOPMENT YATOA MAFUNZO YA KIKODI KWA VIJANA WAJASIRIAMALI ZAIDI YA 30 SHINYANGA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Takribani vijana wajasiriamali zaidi ya 30 katika Manispaa ya Shinyanga wamehitimu mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Shirika la Youth And Women Emancipation (YAWE) kwa kushirikiana na Restless Development.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku mbili, kuanzia Novemba 11 hadi Novemba 12, 2024, yamelenga kuwapa vijana uelewa wa masuala ya kikodi na kuwahamasisha kutambua wajibu wao katika kulipa kodi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya taifa.

Mkurugenzi wa shirika la YAWE Bwana Vicent Laurent, ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewalenga vijana wajasiriamali wenye umri wa miaka 15 hadi 35 wanaojishughulisha na biashara zinazowaingizia kipato, na kwamba nia kuu ya mafunzo hayao ni kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

 "Kuanzia jana tumekuwa na mafunzo kwa vijana wajasiriamali hapa Shinyanga, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao katika kuchangia pato la taifa kupitia kodi,” amesema Laurent.

Katika mafunzo hayo, vijana wamefundishwa faida za kulipa kodi na jinsi gani mchango wao unavyosaidia serikali kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

Bwana Laurent amebainisha kuwa kwa kushirikiana na shirika la Restless Development, wamefanikisha kuleta wataalam kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Polisi Forum na Manispaa ya Shinyanga, ambao wameweza kutoa elimu na mwanga kuhusu fursa za ujasiriamali zinazowezesha vijana kukuza biashara zao.

Bwana Laurent ameongeza kuwa hiyo ni hatua ya awali ya kutoa mafunzo endelevu ambayo yatafuatiwa na mdahalo utakaofanyika hivi karibuni, ambapo vijana watakutana na viongozi wa serikali kujadili changamoto wanazokutana nazo.

“Mafunzo haya ni mwendelezo kwa lengo la kujenga uhusiano bora kati ya serikali na vijana ili waweze kufanya biashara zao kwa mafanikio na serikali ipate mapato,”.

Mafunzo hayo pia yametoa nafasi kwa vijana kuelewa jinsi ya kuzifikia fursa za mikopo zinazotolewa na serikali.

Akizungumza kwa niaba ya afisa maendeleo ya jamii na mratibu wa mikopo Manispaa ya Shinyanga, afisa maendeleo ya jamii kata ya Mjini Brandina Mwinamila amehimiza vijana kuchangamkia mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na serikali, ikiwemo mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani, ambayo asilimia 4 hutengwa kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana, na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Amesisitiza kuwa fursa hizo zimetolewa ili kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwasaidia kujenga biashara imara ambazo zinaweza kuchangia katika kukua kwa pato la taifa.

"Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na ofisi ya Rais Samia Suluhu Hassan imeona umuhimu wa kutoa mikopo hii kama njia ya kuwawezesha vijana kiuchumi hivyo, ni muhimu kwa vijana kuchangamkia fursa hizi ili kuendesha maisha yao na kufikia malengo yao ya kiuchumi." Amesema Brandina.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa KIJANA WAJIBIKA, unaotekelezwa katika mikoa tisa Tanzania bara, kwa lengo la kuwajengea vijana ujasiriamali na kuwahimiza kutimiza wajibu wao wa kikodi.

Mradi huo  ambao ulianza mwaka 2021 unatarajiwa kudumu hadi mwaka 2026, na unalenga vijana wajasiriamali wenye umri kati ya miaka 15 na 35.

Vijana walioshiriki mafunzo haya walionesha shukrani, wakieleza kuwa yamewasaidia kuelewa umuhimu wa kulipa kodi na mchango wa kodi katika maendeleo ya nchi ambapo wameeleza kuwa sasa wana mtazamo mpya kuhusu kodi na watazingatia kulipa kodi kwa wakati ili kuchangia maendeleo.

Mkurugenzi wa Shirika la Youth And Women Emancipation (YAWE), Bwana Vicent Laurent, akizungumza kwenye mafunzo yao leo Novemba 12, 2024.Afisa maendeleo ya jamii Brandina Mwinamila akizungumza kwenye mafunzo hayo leo Novemba 12, 2024.


 

Previous Post Next Post