SMAUJATA MANISPAA YA SHINYANGA YAVUTA HISIA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI NA KUHAMASISHA KAMPENI ZA AMANI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katika jitihada za kupambana na ukatili wa kijinsia na kuimarisha kampeni za amani kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Manispaa ya Shinyanga imeandaa kikao maalum kilichohudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa Dini, vyama vya siasa, wadau wa maendeleo, na wananchi.

Kikao hicho kimefanyika  kwa lengo la kushirikisha jamii katika kampeni safi na zenye ufanisi, huku kikitoa fursa ya kujadili changamoto na mafanikio ya jumuiya hiyo.

Shughuli za SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga

SMAUJATA imejikita katika kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia kwenye kata zote 17 za Manispaa ya Shinyanga, kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii na dawati la jinsia na kwamba inahamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili huku ikiwahimiza wananchi kuwa sehemu ya mabadiliko chanya.

Akisoma taarifa ya jumuiya hiyo makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga Kabizi Gombo amesema mafanikio makubwa yamepatikana, ikiwa ni pamoja na:

Elimu juu ya ukatili iliyowafikia wananchi kupitia semina na mikutano mbalimbali, Ushirikiano na vyombo vya sheria ambapo kesi 11 za ukatili zimefikishwa mahakamani, Namba maalum ya dharura (116) inayowezesha wananchi kuripoti vitendo vya ukatili kwa urahisi.

Ameeleza kuwa SMAUJATA ilizinduliwa kitaifa tarehe 16 Juni 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ambapo katika Manispaa ya Shinyanga, jumuiya hiyo ilianza rasmi tarehe 14 Juni 2024, na imekuwa ikiongozwa na viongozi kutoka ngazi ya kijiji hadi taifa na kwamba lengo kuu ni kuhakikisha jamii inakuwa salama na huru dhidi ya vitendo vya ukatili, hasa katika kipindi muhimu cha uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amesema pamoja na mafanikio hayo SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo Ukosefu wa ofisi ambapo ameeleza kuwa jumuiya hiyo haina sehemu ya kudumu ya kufanyia kazi jambo linalokwamisha utoaji wa huduma bora, Ukosefu wa usafiri amesema shughuli za elimu hufanyika maeneo ya mbali lakini ukosefu wa usafiri unawazuia kufika kwa urahisi, amesema pia wapo baadhi ya vongozi wa SMAUJATA ni watumishi wa umma, hivyo wanapata changamoto ya kushiriki mara kwa mara katika shughuli za shirika.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Telezia Kalunga Alois, aliyekuwa mgeni rasmi ametoa pongezi kwa SMAUJATA kwa juhudi zao katika mapambano dhidi ya ukatili na kuhamasisha kampeni za uchaguzi huru na wa haki.

Ameongeza kuwa mpinga ukatili namba moja ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia jitihada zake za kuanzisha kampeni ya 4R.

"Niwapongeza sana SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga kwa kuandaa kikao hiki. Hata hivyo, naendelea kuwaomba kila mmoja wetu kuwa sehemu ya kupinga vitendo vya ukatili. Mpinga ukatili namba moja ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na ndiyo maana ameanzisha mpango wa 4R. Kwa hiyo, majadiliano haya yanapaswa kuwa ya tija na kuleta maendeleo, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa, ikiwemo kampeni." Amesema Telezia Kalunga Alois.

"Katika mambo ya uchaguzi, kama mnavyoelewa, bila amani na utulivu hakuna jambo linaloweza kufanikishwa. Vyama vya kisiasa ni mali yetu sote, na hakuna kiongozi ambaye hatokani na vyama hivi."

 "Tukizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, hasa kampeni zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni, ili kampeni ziwe za mafanikio, lazima ziwe za uhuru, amani, na haki. Maeneo yasiyo na amani hayawezi kupata maendeleo. Tanzania ni nchi pekee yenye amani, ambapo kila mmoja ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Kwa hiyo, niwaombe vyama vya kisiasa tufanye kampeni zetu kwa amani. Kwa wale waliokwisha jiandikisha, nawasihi kwenda kuchagua kiongozi unayempenda, ukiwa na uhuru wa kufanya hivyo, ilimradi usivunje sheria za nchi." Amesema Telezia Kalunga Alois.

Kikao hicho kimetoa nafasi kwa mjadala, ambapo viongozi wa dini, vyama vya siasa, na watu wenye ulemavu walitoa maoni yao ambapo baadhi ya viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa haki na amani katika kampeni na uchaguzi, huku wakitaka kushirikishwa zaidi katika maamuzi na vikao mbalimbali.

Pia wamesihi viongozi wa serikali na vyama vya siasa kushirikiana kuhakikisha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zinakuwa huru, za haki, na zenye kuzingatia amani.

Miongoni mwa maoni yaliyotolewa ni hitaji la kuwapa watu wenye ulemavu kipaumbele katika mambo yote yanayohusiana na maendeleo ya jamii.

SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga imeonyesha kuwa mapambano dhidi ya ukatili ni suala linalohitaji mshikamano wa kila mmoja, huku ikitoa wito wa kuendeleza jitihada hizo kwa nguvu mpya.

Vyama ambavyo vimeshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Alliance for Change and Transparency Wazalendo (ACT Wazalendo), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), National Convention for Construction and Reform Mageuzi (NCCR Mageuzi), Chama cha Alliance for Democratic Change (CAF), Chama cha Demokrasia Makini (Demokrasia Makini), United Democratic Party (UDP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for Democratic Change (ADC), National Reconstruction Alliance (NRA), Tanzania Democratic Alliance (TADEA) pamoja na Chama cha Kijamii (CCK)

Aidha katika kikao hicho kimehudhuria pia na wawakilishi kutoka  EWURA CCC Mkoa wa Shinyanga

Awali viongozi wa SMAUJATA wakienda kwenda kumpokea mgeni rasmi.









Previous Post Next Post