Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imewataarifu wakazi wa Shinyanga kuhusu kusitishwa kwa huduma ya maji safi kuanzia usiku wa tarehe 1 Novemba 2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kusitishwa kwa huduma hii kunatokana na matengenezo makubwa yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 3 Novemba 2024.
Matengenezo hayo yanahusisha kuziba mpasuko uliotokea kwenye bomba kubwa la chuma linalosambaza maji kutoka kwenye tangi kuu la maji lililopo eneo la Old Shinyanga, Bushushu.
Hata hivyo, maeneo yanayohudumiwa na Bwawa la Ning'hwa, yakiwemo Mwalugoye, Bushushu, Mwasale, na Kambarage, yataendelea kupata huduma ya maji kama kawaida.
SHUWASA imewaomba radhi wananchi kwa usumbufu utakaotokea na kuwataka wakazi wa maeneo husika kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi wakati matengenezo yanaendelea.
Taarifa hii imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma - SHUWASA, tarehe 1 Novemba 2024.