NA NEEMA KANDORO, MWANZA
KUANZA kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) usimamizi wa Mwalo wa Kimataifa wa Samaki Kirumba kumewafanya wadau wa biashara kuitaka serikali kutowazuia kusafirisha abiria na mizigo kwenye chombo kimoja.
Walisema hayo Jijini Mwanza wasafirishaji abiria na mizigo kwenda visiwani kwenye Ziwa Victoria na Jiji la Mwanza kuwa kusafirisha abiria ama mizigo tu kutawafanya washindwe kupata faida kwenye shughuli hiyo.
Mwenyekiti wa Soko la Kimataifa Mwaloni Kirumba Fikiri Magafu alisema wafanyabiashara wanaosafirisha abiria na mizigo inawawia vigumu uendeshaji wake kwani wanashindwa kujaza kufikia kiwango cha ujazo unaotakiwa hivyo wanapata hasara.
“Mathalani kutoka Mwaloni hapa kwenda kisiwa cha Selema wilayani Ukerewe mafuta ya shilingi 482,000 ndiyo yanaweza kutumiwa kwa kwenda na kurudi Mwanza hivyo endapo chombo kitabeba watu 50 wanaolipa 5000 watapata 500,000 hivyo faida hakuna” alisema Magafu.
Mmoja wa wamiliki wa chombo cha usafirishaji majini ndani ya ziwa MV Penda Victoria Baraka Kago ambaye anasafirisha abiria kutoka Mwaloni Kirumba kwenda Kisiwa cha Ghana alisema changamoto anayokabiliana nayo ni kushindwa kujaza hivyo abiria wa kutosha hivyo kuendesha shughuli yake kwa hasara.
Alisema wanapoanza safari hawapiti sehemu zingine kupakia abiria hivyo ameomba serikali iangalie hitaji la kusafirisha kwa pamoja abiria na mizigo kwa kuzingatia ujazo wa boti zao.
Kago alisema kuendelea kwa utaratibu huo unaosimamiwa na TPA utawafanya kushindwa kuendesha biashara zao za usafirishaji ndani ya ziwa hivyo kuathiri biashara zao
Meneja wa TPA Ziwa Victoria Erasto Lugenge alisema wao wamekabidhiwa kusimamia mialo kupitia Tangazo la serikali namba 855 (2023) ili kuimarisha usalama wa abiria na mizigo hivyo hawajasabaisha athari yoyote kwa wafanyabiashara.
Lugenge aliwataka wasafirishaji wa abiria na mizigo katika mwalo huo kuhakikisha kuwa wanapopakia abiria na mizigo wazingatie suala la kuangalia uzito wa vyombo ukoje ili kuepuka kuzidisha
Alisema watatengeneza mwalo huo kuwa na mazingira mazuri kwa usafirishaji wa abiria na mizigo lakini kwa sasa masuala yote ya tozo na kodi inayotozwa katika eneo hilo hawalifanyi.