Na Mapuli Kitina Misalaba
Umoja wa Shirika la Mawakala na Makarani wa Stendi
ya Mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kuzindua mradi wa mahema na viti ambapo mgeni
rasmi alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas
Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Hafla hiyo imefanyika leo Novemba 22, 2024 katika
Stendi ya Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mbunge Katambi ameonesha dhamira ya dhati ya
kusaidia kikundi hicho kwa kutoa msaada wa shilingi milioni moja kwa ajili ya ununuzi
wa viti huku akiahidi kuwapatia spika nne na maikrofoni nne, pamoja na
kuhakikisha wanapata mkopo wa serikali usio na riba ili kuboresha shughuli zao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa
Umoja huo, Bw. Chohe Marwa, ameeleza kuwa kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka
2021 kimeweza kufanikisha mambo makubwa licha ya changamoto zinazowakabili
ambapo umoja huo, wenye wanachama 240, umesaidia kuwaunganisha mawakala na
makarani, kuimarisha mshikamano, na kuondoa ubaguzi kati ya wanachama.
"Tumeweza
kufanikisha kuandaa maadili na miongozo yenye vifungu vitano ambayo ni msingi
wa kazi zetu. Tunaendelea kushirikiana na wadau wa kati na machinga ili
kuboresha huduma katika stendi yetu," amesema Marwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ameeleza changamoto
kadhaa zinazowakabili, ikiwemo uhaba wa viti 200, ukosefu wa mahema matano,
matatizo ya usafiri wa ndani, na ukosefu wa vifaa vya maikrofoni ambapo ameomba
msaada wa serikali na wadau wengine kushughulikia changamoto hizo ili kuboresha
mazingira ya kazi.
Mhe. Katambi, katika hotuba yake, amewapongeza
mawakala na makarani kwa juhudi zao za kuboresha mazingira ya kazi. Aliahidi
kushirikiana nao kuhakikisha changamoto zilizotajwa zinashughulikiwa.
“Tutashirikiana kuhakikisha mnapata mkopo wa
serikali usio na riba. Nitafanya kila jitihada kuhakikisha vifaa vya spika na
maikrofoni mnavyohitaji vinapatikana mapema iwezekanavyo,” amesema Katambi huku
akishangiliwa na umati uliokuwepo.
Wanachama wa umoja huo wamemshukuru Mhe. Katambi kwa
msaada na ahadi zake. “Tumefarijika kuona kiongozi wetu anajali mahitaji yetu
na yupo tayari kushirikiana nasi kuboresha maisha yetu. Tunaamini msaada huu
utafungua njia mpya za mafanikio,” alisema mmoja wa wanachama.
Baada ya hotuba, Mhe. Katambi amezindua rasmi mradi wa mahema na viti ambapo amesema mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa abiria na wafanyabiashara katika stendi ya mkoa na kwamba amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mshikamano na nidhamu katika utekelezaji wa shughuli zao.