UZINDUZI WA KAMPENI KATA YA MWAMALILI NA OLD SHINYANGA: MWENYEKITI WA CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI AONGOZA KWA HAMASA NA MATUMAINI

Leo imekuwa siku yenye hamasa kubwa katika historia ya kampeni za uchaguzi ndani ya Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambapo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ameongoza uzinduzi wa kampeni katika Kata za Mwamalili na Old Shinyanga. Uzinduzi huu umeonyesha dhamira ya chama cha Mapinduzi kuendelea kuwahudumia wananchi kwa maendeleo endelevu.


KATA YA MWAMALILI: KUKAGUA MAENDELEO NA KUHAMASISHA WAGOMBEA
Ziara ya mwenyekiti ilianza Kata ya Mwamalili, ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Twendepamoja. Akiongea baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti aliwasihi wanachama na wagombea kushirikiana kwa karibu na wananchi kutatua changamoto zinazowakabili.

“Ndugu zangu wa Mwamalili, kazi zinazofanyika hapa ni ushahidi wa kazi kubwa ya Chama cha Mapinduzi. Mmejengewa daraja la mto Ng’ong’o, na sasa mnapita bila wasiwasi. Vyumba vya madarasa vinaendelea kujengwa, na hata tunapokumbuka changamoto zilizokuwepo, tunaona jinsi serikali yetu inavyoshughulika na maendeleo ya kila mmoja wetu,” alisema Mwenyekiti huku akiwataka wananchi kuendelea kukiamini chama hicho.

Katibu wa Wazazi Wilaya naye alitoa ujumbe mzito kwa wagombea, akisisitiza uwajibikaji na unyenyekevu kwa wananchi. "Tusipandishe mabega. Wananchi wana imani na nyinyi. Kuwa kiongozi si kuwa bwana bali ni kuwa mtumishi wa wananchi," alisisitiza.


KATA YA OLD SHINYANGA: MKUTANO WA HADHARA WENYE UJUMBE WA MATUMAINI
Baada ya shughuli Mwamalili, Mwenyekiti alielekea Kata ya Old Shinyanga, ambako alipokelewa kwa furaha katika mkutano wa hadhara uliojaa wananchi. Katika hotuba yake, aliwahimiza wananchi kutazama mambo mengi mazuri yaliyofanywa na CCM, huku akiwataka kuwapa nafasi wagombea kusikiliza na kueleza mipango yao.

“Tangu Dr. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, tumeona barabara, madaraja, na huduma mbalimbali zikiboreshwa. Mwamalili na Old Shinyanga ni mifano hai ya kazi nzuri ya serikali ya CCM. Ndugu zangu, wagombea hawa ndio nyinyi wenyewe. Wana maono ya kuendeleza kazi iliyoanzishwa. Tuendelee kushirikiana nao,” alisema Mwenyekiti.


WANANCHI NA VIONGOZI WAHIMIZA HAMASA YA KAMPENI
Diwani wa Kata ya Mwamalili aliwahimiza wagombea kuendeleza mafanikio yaliyofanywa na chama hicho na kuonyesha shukrani kwa Rais Samia kwa juhudi zake kubwa za maendeleo. "Mama yetu Samia tayari ameshapiga kampeni kwa kazi nzuri aliyofanya. Sasa ni zamu yetu kuimarisha mshikamano na kuhakikisha ushindi wa CCM," alisema diwani huyo huku akihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni.

Kwa upande mwingine, wajumbe walionyesha furaha kwa kukaribisha viongozi wa chama na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mshikamano kati ya chama na wananchi.


UJUMBE WA MWENYEKITI: CHAMA CHA MAPINDUZI NI TEGEMEO LA WATANZANIA
Mwenyekiti alimalizia kwa kuwahimiza wananchi kuendelea na imani kwa CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kimeonyesha uwezo wa kushughulikia changamoto na kuleta maendeleo. “Maendeleo ni mchakato. Tuliyoyafanya ni mengi, lakini bado kuna zaidi tunalolifanya. Tushirikiane, tuendelee na moyo wa matumaini,” alihitimisha.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mhe. Anord Makombe akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Twendepamoja Kata ya Mwamalili.

 

Previous Post Next Post