WAKAZI WA SALAWE WAHIMIZWA KUSHIRIKI KAMPENI ZA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Wakazi wa Kata ya Salawe, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wamehimizwa kushiriki kampeni za vyama vya siasa zinazotarajiwa kuanza leo, Novemba 20 hadi Novemba 26, 2024, kwa lengo la kusikiliza sera ili kuchagua viongozi wenye nia ya kuleta maendeleo.

Diwani wa Kata ya Salawe, Mhe. Joseph Buyugu, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ametoa wito huo Novemba 19, 2024, wakati akifungua bonanza la michezo lililoandaliwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, katika viwanja vya Stendi ya Mabasi Salawe.

Mhe. Joseph Buyugu, amewataka wananchi wa Salawe kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni za vyama vya siasa zinazotarajiwa kuanza Novemba 20, 2024 ambapo ameeleza kuwa ushiriki wa wananchi katika kampeni ni muhimu ili kusikiliza na kupima sera za viongozi wa vyama mbalimbali kabla ya uchaguzi wa Novemba 27, 2024.

"Kuanzia tarehe 20, tutaanza kampeni za vyama vya siasa kwa vyama vyote. Nitoe rai, nawaomba sana wananchi mjitokeze kwa wingi kusikiliza sera za viongozi wa vyama mbalimbali. Tunasisitiza hili ili wananchi waweze kupima sera za viongozi hao na kuchagua kiongozi mnayemtaka tarehe 27, mwezi huu, kulingana na sera zake.

"Ni muhimu kuwapima viongozi hawa kwa sera zao ili waweze kuwaletea maendeleo na kuondoa kero zenu. Kusikiliza sera ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi, hivyo nawaomba mjitokeze kwa wingi," amesema Mhe. Buyugu.

Bonanza hilo limejumuisha michezo ya aina mbalimbali, ikiwemo kukimbia na magunia, kuvuta kamba, kufukuza kuku, na mashindano ya kunywa soda.

Mabonanza hayo yameendelea kufanyika katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kwamba ni sehemu ya juhudi za kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa ushiriki wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Salawe wamepongeza kufanyika kwa bonanza hilo ambapo wamesema kuwa Michezo hiyo ni burudani, lakini pia ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe muhimu wa kushiriki uchaguzi.

Kampeni za vyama vya siasa zinatarajiwa kufanyika kwa siku saba, zikilenga kuelimisha wananchi kuhusu sera za vyama na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni tukio muhimu katika kuimarisha demokrasia na maendeleo ya jamii, huku wakazi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi katika siku ya uchaguzi.

Diwani wa Kata ya Salawe, Mhe. Joseph Buyugu, akizungumza kwa niaba ya  Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, katika bonanza la Michezo.

Diwani wa Kata ya Salawe, Mhe. Joseph Buyugu, akizungumza kwa niaba ya  Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, katika bonanza la Michezo.
Mchezo wa watoto ukiendelea






Previous Post Next Post