Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana akifungua mkutano huo mkoani Arusha
Happy Lazaro, Arusha
.WADAU wa utalii nchini wametakiwa kuweka mikakati endelevu katika kukuza Sekta ya Utalii na Ukarimu hususan katika nyanja za utunzaji wa mazingira na ustawi wa jamii.
Aidha wametakiwa kutumia teknolojia za kidijitali na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa maendeleo endelevu na ustawi wa Sekta ya Utalii.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana wakati akifungua Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kuunganisha wanataaluma na wadau wa Utalii na Ukarimu katika Nchi Zinazoendelea uliofanyika jijini Arusha.
Dkt Chana amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utalii ambapo kupitia mkutano huu wanataaluma watatoa matokeo ya tafiti na mifumo ya kinadharia inayohitajika kuelewa changamoto kubwa zilizopo.
“wadau wa sekta watatoa ufahamu wa vitendo kupitia uzoefu wao katika kazi na biashara za utalii ili kusaidia kuleta uvumbuzi, kuimarisha mafunzo, na kuongeza ajira” amesema . Chana.
Amefafanua kuwa ili Sekta ya Utalii na Ukarimu iendelee ni vyema kukawa na hatua za kulinda mazingira kwa kuhifadhi misitu, wanyamapori, na rasilimali za baharini pamoja na kuwepo na ushirikishwaji wa jamii kwa kuwepo na utalii wa kijamii.
Aidha Chana amefafanua kuwa msisitizo juu ya teknolojia katika mkutano huo ni muhimu hasa katika kujadili mada za Mawasiliano ya kidigitali na matumizi ya kompyuta katika Ukarimu na Utalii akitolea mfano kutalii kidigitali na kuwa na vyumba vya hoteli vinavyoendeshwa kidigitali.
Ameongeza kuwa, mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ya Utalii yanapelekea kufikiria upya kuwa, utalii sio tu njia ya kufikia malengo bali unaambatana na utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Florian Mtey amesema kuwa wakati dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kuwepo na mijadala endelevu kuhusu namna ya kukabiliana nayo pamoja na namna ya kukuza utalii na ukarimu kwa kutumia mbinu rafiki wa mazingira, teknolojia za kidijitali, na fursa zingine zilizopo.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Mikakati ya Utalii Endelevu na utalii wa bahari kufikia malengo endelevu na ya kidigitali, yaani “Green and Blue Tourism Strategies Towards Sustainability and Digitalization,” ulioandaliwa na NCT kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane kutoka nchini Afrika Kusini na Chuo cha Utalii cha Kenya kutoka nchini Kenya.
Aidha mkutano huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa utalii kutoka Kenya, Afrika Kusini, Zambia, Malawi, Botswana, Marekani, Finland, Korea Kusini, India, Sweden, Ethiopia, Ujerumani, China, Uholanzi pamoja na Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii,Wakuu wa Taasisi za Elimu kutoka Nchi mbalimbali, Wawakilishi kutoka Mashirika ya Utalii na Wawakilishi kutoka Vyama vya Usafiri wa Anga Nchini.