Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewataka Watanzania kuwaenzi mashujaa kwa kuendeleza utu, amani na ubinadamu walioupigania ili kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.
Ametoa kauli hiyo leo alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa waliopigania Vita ya Kwanza ya Dunia iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Novemba 10,2024.
“Katika Siku hii ya Kumbukumbu, sio tu kwamba tunaadhimisha maisha yao bali tunafanya upya dhamira yetu ya kushikilia kanuni walizozisimamia, ambazo ni dunia yenye amani, ubinadamu na utu” Mhe. Chana amesisitiza.
Amefafanua kuwa katika kumbukumbu za mashujaa hao, jamii zinahimizwa kulinda amani waliyoipigania kwa ujasiri, na kuendeleza urithi wao kwa kujenga madaraja ya maelewano na ushirikiano kuvuka mipaka ya nchi na kusisitiza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali za amani duniani, Tanzania imesimamia imani yake kwamba suluhu za migogoro ya kudumu hazitokani na mtutu wa bunduki bali kupitia diplomasia, mazungumzo na maelewano.
Aidha, ameongeza kuwa zinahitajika juhudi za pamoja ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za kidunia kama mabadiliko ya tabia nchi, umaskini, ukosefu wa chakula, magonjwa ya milipuko na ukosefu wa usalama mtandaoni, kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo vinarithi ulimwengu ambao sio tu wa amani bali uthabiti na wa haki.
Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kuziomba Jumuiya za Kimataifa kuzidisha juhudi za kuleta maazimio ya amani huku akiwapongeza mashujaa waliojitolea kudumisha amani.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani na Ubalozi wa Uingereza nchini, yamehudhuriwa na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Thomas Terstegen, Mwakilishi wa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo Ubalozi wa Uingereza, Kemi Williams, Waheshimiwa Mabalozi na Makamishna Wakuu, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Maafisa wa Serikali.