Na Mapuli Kitina Misalaba
Ligi ya XMASS CUP imeanza rasmi
Novemba 28, 2024, katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini ambapo mashindano hayo
yanashirikisha timu 16, zikiwemo timu saba kutoka kata ya Salawe na timu nyingine
kutoka kata jirani.
Katika mechi ya ufunguzi, timu ya
Kano FC imetoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mahembe FC.
Kwa mujibu wa mwandaaji na mdhamini
wa ligi hiyo, Makamba Mussa Lameck, ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya
MCL inayojishughulisha na biashara ya nafaka na mazao mengine, amesema ligi
hiyo inalenga kuibua vipaji na kutoa fursa za maendeleo kwa vijana kupitia
michezo.
“Lengo kuu ni kuibua vipaji, kujenga
nidhamu kwa wachezaji, na kuwapa vijana fursa ya kushiriki mashindano makubwa
zaidi. Tunaamini kupitia ligi hii, tunaweza kutengeneza timu imara inayoweza
kushiriki ngazi za juu, hata Ligi Kuu.”
Pia aliongeza kuwa mashindano hayo
hayana kiingilio, hivyo kuwa fursa kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa zao wakati
wa mechi.
“Mungu
ni mwema; tumeanza ligi yetu salama, lakini pia tunaiona dhamira ya watu
kushiriki kwenye ligi hii.”
“Lengo kubwa la ligi hii ni kuibua vipaji
mbalimbali. Ukiangalia, Kata ya Salawe ina timu takriban nane, lakini pia
tunazo timu za kata zingine ndani ya Wilaya yetu na hata Wilaya jirani ya
Misungwi.”
“Vijana wetu hawa wamekuwa wakizunguka kwenye
ndondo mbalimbali kwa lengo la kujipatia kipato. Nimeona si vibaya kuanzisha
ligi itakayowaletea ushindani ndani ya Wilaya, ngazi ya Mkoa, na pengine hata
kushiriki Championship. Mungu akipenda, tunaweza hata kufikia Ligi Kuu. Ndiyo
maana kwenye ligi hii tumekusanya timu kutoka kata na Wilaya tofauti kwa lengo
la kuwa na muunganiko wa timu moja imara itakayowawezesha vijana kufikia
malengo yao.” amesema Makamba
“Lengo
lingine ni kutoa fursa kwa watu mbalimbali, kwa kuwa ligi hii haina kiingilio.
Wafanyabiashara wanapata nafasi ya kuuza bidhaa zao ili kujipatia kipato. Kama
inavyofahamika, michezo ni amani, afya, umoja, na burudani. Hivyo, nia yetu ni
kuwaunganisha watu pamoja.”
“Timu
au vijana wanaoshiriki kwenye ligi hii, ninawasihi mafanikio yoyote yanahitaji
nidhamu. Wachezaji hawa ni vijana wenye umri mdogo na wana safari ya kuendelea
kujenga maisha yao. Nidhamu pamoja na vipaji walivyojaliwa na Mungu vinaweza kuwafikisha
sehemu nzuri. Naomba timu zote 16 ziimarishe nidhamu, kwa kuwa mpira ni ajira,
na nidhamu ndiyo njia sahihi ya kufanikisha ajira hiyo.”amesema
Makamba
Kwa upande wake, msimamizi wa
mashindano, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, amefafanua kuwa mshindi wa
kwanza wa XMASS CUP atajinyakulia zawadi ya shilingi milioni moja, mshindi wa
pili shilingi laki tano, na mshindi wa tatu shilingi laki mbili na kwamba
zawadi za mchezaji bora na golikipa bora zitakuwa shilingi 50,000 kila mmoja.
Mashindano hayo yataendelea kwa
mfumo wa mtoano ambap timu zilizoshinda katika hatua ya awali zitapanda hadi
robo fainali, kisha nusu fainali, na hatimaye fainali itakayofanyika Disemba
17, 2024, katika uwanja wa Shule ya Msingi Mangu, kijiji cha Songambele,
Salawe.
Mgeni rasmi katika
uzinduzi wa XMASS CUP ni mkuu wa kituo cha Polisi Salawe OCS Richard Kapongo
ambaye amewasihi wachezaji
kudumisha nidhamu na kuzingatia kuwa michezo ni sehemu ya ajira ambapo pia
amesisitiza michezo hiyo kuwa ya amani.
Timu zinazoshiriki ni:
- Kano FC
- Mahembe FC
- Sec Combine FC
- Isenengeja FC
- Machongo FC
- Mwabenda FC
- Salawe FC
- Solwa FC
- Beya FC
- Ngubalu FC
- Ikonongo FC
- Mwawile FC
- Mwagiligili FC
- Mahando FC
- Modern FC
- Mwasenge FC
Aidha wachambuzi wa ligi hiyo ni Samwel Sambiji
(Mkongo) na Baba Paroko
Mashindano haya yanatarajiwa kuvutia
umma na kuleta burudani ya kipekee msimu huu wa Krismasi. Endelea kufuatilia
taarifa za matukio na matokeo kupitia MISALABA MEDIA.
Mgeni rasmi katika
uzinduzi wa XMASS CUP ni mkuu wa kituo cha Polisi Salawe OCS Richard Kapongo
akifungua mashidano hayo Novemba 28, 2024.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa XMASS CUP ni mkuu wa kituo cha Polisi Salawe OCS Richard Kapongo akifungua mashidano hayo Novemba 28, 2024.
TAZAMA VIDEO
MAGOLI YOTE TAZAMA VIDEO HII