Wanafunzi wanaotarajiwa kuanza elimu ya sekondari wameaswa kupokea kwa mtazamo chanya masomo ya amali watakayoanza kusoma mwakani, kwani yamelenga kuwaandaa kuwa na maarifa makubwa ya stadi za kazi.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Udhibiti Ubora wa Elimu Kanda ya Ziwa, Lucy Nyanda, kwa wanafunzi 54 waliohitimu darasa la saba katika Shule Maalumu ya Msingi Claud iliyopo Jijini Mwanza, ambao wote wamepata ufaulu wa daraja la kwanza kwenye mitihani yao.
Nyanda alisema mitaala hiyo mipya itakuwa jawabu kwa wanafunzi wenye vipaji katika fani yoyote, kwani itawawezesha kujifunza kwa muda mrefu na kuwa mahiri, hivyo kufanya vizuri kivitendo.
"Tayari mkoani Mwanza, elimu ya amali imeshaanza kufundishwa katika baadhi ya shule za sekondari na kuonesha mafanikio makubwa ya kuwaandaa wanafunzi kuwa na stadi za maisha," alisema Nyanda.
Aidha, alibainisha kuwa mwanafunzi anayependa masomo ya sayansi au ufundi ataweza kujifunza mapema kuanzia sekondari, hali itakayomfanya kuwa mahiri zaidi katika eneo husika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Victor Raphael, alisema ili kuwaendeleza wanafunzi hao waliohitimu darasa la saba, shule hiyo mwakani itaanzisha sekondari itakayofundisha mitaala mipya kwa umahiri.
Alisema ushirikiano waliopata kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao umechangia mafanikio makubwa ya wanafunzi hao, ambao wote wamepata daraja la kwanza.
Naye Padre Felix Magobe alisema kuanzishwa kwa kidato cha kwanza kwa wasichana kutachangia kuandaa jamii yenye maadili, akisisitiza kuwa mwanamke ana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii yake.