ASKOFU SANGU ATOA WITO KWA JAMII KUWALINDA WATOTO DHIDI YA VITENDO VYA UKATILI


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ametoa wito kwa jamii nzima kuwalinda na kuwatunza watoto.


Ametoa wito huo kupitia Misa ya Kijimbo ya sikukuu ya watoto mashahidi iliyofanyika leo katika Kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga, ambayo ni sehemu ya kumbukumbu ya watoto waliouawa kwa amri ya Mfalme Herode siku chche baada ya kuzaliwa kwa Kristo.


Askofu Sangu, amewataka wazazi, walezi na jamii nzima kuwajibika kuwalinda na kuwatunza watoto, pamoja na kufuatilia kwa karibu mienendo yao ili kuwaepusha na mambo yote ambayo yanaathiri ustawi wao, kupitia yale wanayojifunza kwa wengine au vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.


Amebainisha kuwa, Kanisa Katoliki litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kupinga na kuzuia aina zote za ukatili kwa watoto, ambavyo ni pamoja na unyanyasaji wa kingono.


Askofu Sangu ameikumbusha jamii ya wakristo kuhakikisha inawalea watoto kwa kuzingatia misingi ya imani yao, pamoja na kuwaombea ili Mungu awalinde dhidi ya mambo yote mabaya yanayotishia ustawi wao.


Misa ya sikukuu ya watoto mashahidi imetanguliwa na maandamano maalum ya watoto yaliyongozwa na Askofu Sangu kutoka katika Parokia ya Moyo safi wa Maria Shinyanga mjini mpaka Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo, ambayo yalikuwa yamebeba ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo kupinga ukatili kwa watoto.


Jimboni Shinyanga kwa mwaka huu Misa hiyo ya sikukuu ya watoto mashahidi, imehudhuriwa na watoto zaidi ya 2,500 kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo, ambapo kwa utaratibu uliowekwa, Askofu husali, kuzungumza, kula na kusherekea pamoja na watoto.


Sikukuu ya watoto Mashahidi huadhimishwa na Kanisa Katoliki kote duniani kila ifikapo Desemba 28, ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi watoto wa kiume wa kuanzia miaka miwili na kushuka chini waliouawa kwa amri ya Herode aliyekuwa Mfalme wa Yudea siku chache baada ya kuzaliwa kwa Kristo, ambapo kwa mujibu wa maandiko matakatifu, hatua hiyo ililenga kumwangamiza mtoto Yesu aliyemhofia kutwaa madaraka yake.
Previous Post Next Post