ASKOFU SANGU KESHO KUADHIMISHA MISA YA KIJIMBO YA SIKUKUU YA WATOTO MASHAHIDI

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Jumamosi tarehe 28.12.2024, ataongoza Misa ya kijimbo ya sikuu ya watoto mashahidi, ambayo ni kumbukumbu ya watoto waliouawa kwa amri ya Mfalme Herode siku chache baada ya kuzaliwa kwa Kristo.

Misa hiyo itatanguliwa na maandamano maalum ya watoto ambayo yataanza saa 3:00 asubuhi  yakiongozwa na Askofu Sangu kutoka katika Parokia ya Moyo safi wa Maria Shinyanga mjini mpaka Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo, na yatakuwa na  ujumbe unaohusu masuala mbalimbali  ikiwemo kupiga ukatili kwa watoto.

Baada ya maandamano hayo kuwasili katika Kanisa kuu Ngokolo, saa 4:00 asubuhi Askofu Sangu ataadhimisha Misa takatifu ya Sikukuu ya watoto Mashahidi ambayo itahudhuriwa na watoto zaidi ya 2,500, kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo, ambapo kwa utaratibu wa Jimbo la Shinyanga, siku hiyo Askofu husali, kuzungumza, kula pamoja na kusherekea na watoto.

Kupitia Misa hiyo ya sikukuu ya watoto mashahidi, Askofu Sangu pia atazindua kijimbo Jubilei ya miaka 2025 ya Ukristo duniani.

Sikukuu ya watoto Mashahidi huadhimishwa na Kanisa Katoliki kote duniani kila ifikapo Desemba 28, ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi watoto wa kiume  wa kuanzia miaka miwili na kushuka chini waliouawa kwa amri ya Herode aliyekuwa Mfalme wa Yudea siku chache baada ya kuzaliwa kwa Kristo, ambapo kwa mujibu wa maandiko matakatifu, hatua hiyo ililenga kumwangamiza mtoto Yesu aliyemhofia kutwaa madaraka yake.

Previous Post Next Post