ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI KWA WAKULIMA WA BUSTANI NA MAZAO YA MPUNGA , MAHINDI KIJIJI CHA SONGAMBELE MKOANI SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Watoto hususani wanafunzi katika mkoa wa shinyanga wako katika hatari ya kupata utapiamlo na kusitisha masomo kutokana na ukosefu wa chakula cha kutosha kufuatia jamii mkoani humo kushindwa kuzalisha chakula cha kutosha kwa sababu za ukame.

Wakizungumza na waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari za vijijini nchini Tanzania (RUJAT) baadhi ya wakulima wa kijiji cha Songambele, kata ya Salawe, wilaya ya Shinyanga Vijijini, wanakabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hali inayozidisha matishio ya kiusalama na hofu ya kutokea kwa baa la njaa na ongezeko la umasikini.

Wamebainisha kuwa mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha kubadilika kwa majira ya mvua na kupungua kwa mvua za kutosha, kupungua kwa mavuno, na changamoto za maji ya umwagiliaji, hasa wakati wa kiangazi.

Samwel Gulaka, mkazi wa kitongoji cha Machongo, anaeleza jinsi mabadiliko haya yameathiri familia yake na kupelekea watoto kuanza kuzorota kwenye mahudhurio shuleni na kuyumba kwa afya. 

"Mimi ni mkulima wa bustani kwa zaidi ya miaka kumi, kilimo hiki kimekuwa chanzo cha kipato changu lakini tangu mwaka 2022, hali imekuwa mbaya ambapo Mwaka huo, mazao yangu yalinyauka kwa sababu ya ukosefu wa maji ya kumwagilia nilitumia gharama kubwa lakini sikuweza kupata mavuno kabisa hali hiyo ilisababisha njaa na matatizo makubwa ya kifamilia," anasema Gulaka kwa masikitiko makubwa.

Gulaka anategemea kilimo cha bustani kwa mahitaji yote ya familia, ikiwa ni pamoja na kununua chakula na kusomesha watoto hata hivyo, kuanzia mwaka 2022, maji yamekuwa yakikauka kila kiangazi, na hali hii imelazimisha baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao fulani. "Tunaomba serikali na wadau wengine watujengee kisima cha maji au malambo makubwa ambayo yatatuwezesha kupata maji ya uhakika wakati wote wa Bustani," anaomba Gulaka.

Kwa upande wake Piter Lutonja, mkazi wa Songambele, anaeleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimeathiri uwezo wake wa kuhudumia familia. 

"Kilimo cha bustani kimekuwa changamoto Nyanya ambazo zamani nilikuwa napata milioni mbili kwa miche 2000, sasa nalazimika kuishia na shilingi laki tano tu hali ya ukosefu wa maji wakati wa kiangazi, kutoka Juni hadi Septemba, inaharibu mazao na kutufanya tupate hasara kubwa," anasema.

Lutonja anasema changamoto hizo zimemlazimu kufanya vibarua ili kulisha familia na kusomesha watoto.

"Kuna wakati nilishindwa kabisa kusomesha mtoto wangu kwa sababu sikuwa na pesa baada ya mazao kuharibika Kilimo cha bustani, ambacho kilikuwa cha faida kubwa, sasa kinaonekana kuwa mzigo," anaeleza kwa uchungu.

Simon Mayala, mkulima wa mpunga na mahindi kutoka kitongoji cha Kituli, anasema kuwa mvua zisizotabirika zimepunguza mavuno kwa kiasi kikubwa. "Zamani nilikuwa napata gunia 30 kwa hekari mbili za mpunga, lakini sasa napata gunia 10 tu. Mahindi, ambayo zamani nilivuna gunia 20 kwa hekari mbili, sasa naishia na gunia tano mavuno haya hayakidhi hata chakula cha familia, achilia mbali mahitaji mengine kama ada za shule," anasema Mayala.

Shija Ntemi, mkulima mwingine wa mahindi, anasema mwaka 2023 alipata gunia mbili tu kutoka hekari saba alizolima hali hiyo ilimfanya abadilishe mazao na kulima mihogo, ambayo ilimletea gunia 28 hata hivyo, bado hajafikia malengo yake ya kuendesha familia na kusomesha watoto saba. "Nikiwa na watoto watatu sekondari na wengine shule ya msingi, najikuta nikikopa mara kwa mara ili kuhakikisha wanasoma Kilimo ndiyo tegemeo letu, lakini hali ya mvua imekuwa tatizo kubwa," anasema Ntemi.

Hali hii imesababisha baadhi ya wakulima kubadili mbinu na kuanza kutumia teknolojia za kisasa ambapo George Lameck, mkulima wa kisasa wa mpunga na mahindi, anasema kuwa kilimo cha kisasa kimekuwa na faida kubwa licha ya changamoto za tabianchi. "Mwaka 2023, nililima hekari moja ya mpunga na kupata gunia 25 Kilimo cha kisasa kinanisaidia kutumia mbegu za muda mfupi na kupata mavuno mengi," anasema Lameck, akihimiza wakulima wengine kuachana na kilimo cha jadi.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Songambele, Bi. Evalina Isack, anasisitiza umuhimu wa kilimo cha kisasa. "Mabadiliko haya ya tabianchi yamekuwa yakiwaathiri sana wakulima wanaotegemea kilimo cha jadi, nawashauri wakulima kutumia pembejeo za kisasa ili kuongeza mavuno na kukabiliana na hali ya hewa isiyotabirika," anasema Evalina.

Kwa upande wake, Afisa kilimo wa kijiji hicho Bi. Atules Wilfred anashauri wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame kama mtama, alizeti, viazi, na mihogo ili kupunguza athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabianchi.

 Kupitia msaada wa serikali, mashirika, na wadau wengine, wakulima wa Songambele wanaweza kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo na kujenga maisha bora kwa familia zao.

Miongoni mwa Mashirika yanayojihusisha na utoaji wa elimu kuhusu masuala ya kilimo endelevu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ni Chama cha waandishi wa habari za Vijijini (RUJAT), Shirika la We-World la nchini Italia, shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa (WFP) shirika la kilimo na chakula duniani (FAO) pamoja na Wizara mtambuka za serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania hususani Kilimo, Afya, Mazingira, Mifugo na Umwagiliaji.

Simon Mayala, mkulima wa mpunga na mahindi kutoka kitongoji cha Kituli kijiji cha Songambele akiendelea na shughuli

Simon Mayala, mkulima wa mpunga na mahindi kutoka kitongoji cha Kituli kijiji cha Songambele akiendelea na shughuli


 

Previous Post Next Post