Picha ya pamoja Beya FC kutoka Salawe washindi wa mechi ya leo.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Ligi ya Makamba Lameck maarufu kama Krismas CUP
inaendelea kwa kasi katika uwanja wa Mhangu, ambapo leo Beya FC ya Salawe imeibuka
mshindi dhidi ya Ngubalu FC ya Mwanza kwa bao moja la pekee lililofungwa na
Robert Clement dakika ya 37.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Makamba Mussa
Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka,
yamelenga kuibua vipaji vya michezo mkoani Shinyanga huku yakichangia
mshikamano wa kijamii.
Akizungumza baada ya mechi, Mwenyekiti wa Sungusungu
wa kijiji cha Songambele, kata ya Salawe, Moto Mussa Kalamji, amepongeza juhudi
za kuandaa ligi hii ambapo ameeleza kuwa mashindano hayo siyo tu burudani kwa
wakazi bali pia ni jukwaa muhimu la kuinua vijana wenye vipaji.
“Ligi hii ni fursa ya kipekee kwa vijana kuonyesha
uwezo wao. Michezo ni sehemu ya ajira na maendeleo, hivyo nawahimiza wachezaji
wote kujituma zaidi,” amesema Moto huku akiwahakikishia usalama wa wananchi
katika mashindano hayo.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock
Kijida, amefafanua kuwa mechi inayofuata itazikutanisha timu za Ikonongo FC na
Mwawile FC kesho.
Ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea
kujitokeza kwa wingi kufurahia michezo na kuunga mkono juhudi za kuendeleza
vipaji vya vijana.
Mwenyekiti wa Sungusungu wa kijiji cha Songambele,
kata ya Salawe, Moto Mussa Kalamji, akipongeza uwepo wa ligi hiyo huku
akiwahakikishia wananchi usalama.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock
Kijida, akizungumza leo Disemba 3, 2024.