Morogoro
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Mizengo Pinda amewataka wahitimu wa chuo cha Ardhi Morogoro kuachana na vitendo vya rushwa katika kutekeleza utaalamu wa taaluma yao kwa manufaa mapana na kustawisha sekta ya ardhi nchini.
Mhe. Pinda ameyasema hayo leo tarehe 06 Novemba 2024 katika Mahafali ya 43 ya chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) yaliyofanyika Katika viwanja vya chuo hicho Mkoani Morogoro
Aidha mhe Pinda amewaasa wahitimu hao kuzingatia kanuni na sheria zilizowekwa katika kutekeleza majukumu ya sekta ya ardhi na kuepuka migogoro isiyo ya lazima sambamba na kuacha utashi binafsi katika kushughulikia mambo ya Ardhi.
Mbali na hilo Naibu Waziri Mhe Pinda amewakumbusha wahitimu hao kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya Ukimwi kwa sababu bado wanahitajika sana kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande mwingine wao Esther Joseph Haule na Kelvin Mayao wahitimu wa kozi ya mipango miji katika chuo hicho wameahidi kutumia elimu yao kutatua migogoro ya ardhi kwa ajili ya kustawisha sekta hiyo
Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kilianzishwa mwanzoni mwa mwaka 1958 kikiwa na lengo la kutoa elimu ya mafunzo ya Utafiti wa masuala ya Ardhi (Training Land Surveying ) ambapo mpaka sasa kimefanya Jumla ya Hafla za Mahafali 43.