Na Mapuli Kitina Misalaba
Watoto wawili wamefariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya fisi
katika Kata ya Igaga, Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, huku watu wengine
sita wakijeruhiwa.
Misalaba Media imezungumza na Mkuu wa Wilaya ya
Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, ambaye amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa
fisi huyo alitokea katika maeneo ya hifadhi ya milima ya Mawa na kuingia katika
makazi ya watu mnamo Desemba 12, 2024, majira ya saa tano hadi saa saba mchana.
Kwa mujibu wa maelezo yake, fisi huyo aliendelea
kuvamia makazi ya watu ambapo alimjeruhi mama mmoja na kisha kuingia ndani ya
nyumba na kuwaua watoto wawili, Mussa Philip (miaka nane) na Stephano Philip
(miezi minane), ambao ni wa familia moja.
“Fisi
huyo alionekana ghafla majira ya saa tano hadi saa saba mchana, akitokea maeneo
ya hifadhi ya milima ya Mawa. Hadi sasa bado hatujafahamu kwa nini alitoka kule
na kuja maeneo ya wananchi nyakati hizi.”
“Baada
ya kufuatilia, tumegundua kuwa fisi huyo alikuwa amejeruhiwa. Kila alipokutana
na mtu, alimshambulia. Alianza kumshambulia mtoto wa kike aliyekuwa akichunga
ng’ombe karibu na nyumbani. Binti huyo alipiga kelele, na mzee mmoja alijaribu
kumuokoa, lakini naye akajeruhiwa.”
“Fisi
huyo aliendelea hadi kwenye makazi ya watu kijijini kabisa. Alimvamia mama
mmoja mwenye watoto wawili. Watoto hao walikuwa ndani ya nyumba, na mama huyo
alipokuwa akijaribu kumzuia fisi, naye alijeruhiwa. Baadaye, fisi huyo aliingia
ndani ya nyumba na kuwashambulia watoto hao wawili, hali iliyosababisha vifo
vyao.”amesema DC Mkude
Jeshi la wanyamapori lilifika eneo la tukio haraka
mara baada ya taarifa kutolewa, lakini fisi huyo alishauawa na wananchi kabla
ya askari kufika.
“Sasa,
hatua tulizochukua ni pamoja na kuwaita askari wa wanyamapori, ambapo watatu
walifika mapema. Pia, maafisa wa wanyamapori wa Halmashauri walikuwepo. Hata
hivyo, wananchi walichukua hatua ya kumtoa fisi huyo ndani ya nyumba na
kumshambulia hadi kufa. Askari walipofika eneo la tukio, walikuta fisi tayari ameuawa.”
“Baada
ya tukio hilo, serikali imeamua kushiriki kwenye msiba wa watoto wawili
waliopoteza maisha. Vilevile, tumeanza operesheni ya kuwinda fisi katika maeneo
hayo ili wananchi wakae salama. Operesheni hiyo ilianza jana usiku na
itaendelea mpaka hali itakapokuwa shwari zaidi. Hadi sasa, hakuna fisi mwingine
aliyeripotiwa kuonekana.”amesema DC Mkude
Aidha, majeruhi sita wa tukio hilo wamesafirishwa hadi hospitali ya mkoa kwa matibabu zaidi. “kwa upande wa majeruhi sita, baada ya kuona hali zao si nzuri, tumewapa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa kwa matibabu sahihi na uangalizi wa madaktari bingwa. Lengo ni kuhakikisha wanarejea katika hali yao ya kawaida haraka iwezekanavyo.”
Mhe. Mkude ametoa wito kwa wananchi kuchukua
tahadhari katika kipindi hiki ambapo wanyama wakali wameanza kuonekana karibu
na makazi ya watu. “Ni muhimu watoto wawe nyumbani mara baada ya kutoka shuleni
na kupewa majukumu yanayoweza kufanyika katika mazingira salama,” amesisitiza
Mkude.
Operesheni ya kuwinda fisi wengine imeendelea, na
hadi sasa hakuna mnyama mwingine aliyeripotiwa kuonekana ambapo mazishi ya
watoto waliofariki yanafanyika leo, huku serikali ikishirikiana na familia ya
marehemu kuhakikisha taratibu zote zinaenda salama.