Na Mapuli Kitina Misalaba
Robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Makamba Lameck
(Krismas Cup) imefanyika leo Desemba 7, 2024 kwa ushindani mkali kati ya
Sekondari Combine FC na Kano FC, ambapo Kano FC wameibuka washindi kwa bao 1-0
lililofungwa na Emmanuel Mchenya dakika ya 57.
Akizungumza kwa niaba ya msimamizi wa mashindano
hayo, Placid Thomas amesema ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mwingine wa
robo fainali kati ya Beya FC na Ikonongo FC (Mahakama).
Ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi na wapenzi
wa michezo kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya wachezaji wa Shinyanga.
Kocha wa Sekondari Combine FC amepongeza juhudi za
vijana wake, akisema kuwa mashindano haya ni chachu ya kuwaandaa kwa mashindano
mengine makubwa.
Pia, amemshukuru Makamba Lameck kwa kuwawezesha
vijana kushiriki mashindano hayo na kumuomba aendelee kuandaa matukio kama haya
katika siku zijazo.
Mashindano ya Krismas Cup, yanayodhaminiwa na
Makamba Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya
nafaka, yanalenga kukuza vipaji vya michezo mkoani Shinyanga.
Fainali za mashindano hayo zinatarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba 2024, huku hamasa ikiendelea kuongezeka miongoni mwa timu shiriki na mashabiki wa michezo.