Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, leo Jumanne tarehe 17.12.2024, amekutana na Mapadre wa Jimbo Katoliki Shinyanga ambao aliwapa daraja la Ushemasi au Upadre na kufanya nao mazungumzo ya faragha.
Kardinali Pengo akiwa na mwenyeji wake Mhashamu Liberatus Sangu, Askofu wa Jimbo la Shinyanga, amekutana na Mapadre hao katika makazi mapya ya Askofu yaliyopo eneo la Ibadakuli nje kidogo ya mji wa Shinyanga.
Baada ya mazungumzo hayo, Kardinali Pengo ameshiriki chakula cha pamoja na Mapadre pamoja na wawakilishi wa waamini katika Parokia ya Lubaga.
Kesho Jumatano, atakutana kwa mazungumzo na Mamonsinyori watatu wa Jimbo la Shinyanga katika Parokia ya Buhangija, kabla ya kushiriki Ibada ya Masifu ya jioni katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya utolewaji wa daraja la Ushemasi kwa frateri Deusdedith Nkandi.
Kardinali Pengo yupo Jimboni Shinyanga kwa siku nne, ambapo pamoja na mambo mengine, keshokutwa Alhamisi ataongoza Misa takatifu na kumpa daraja la Ushemasi Frateri Deusdedith Nkandi wa Parokia ya Buhangija, Jimbo la Shinyanga.