KATIBU WA SMAUJATA KANDA YA ZIWA DANIEL KAPAYA ATOA WITO WA ULINZI WA WATOTO MTANDAONI

Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Bw. Daniel Patrick Kapaya, akizungumza kwenye mahafali hayo katika shule ya awali Marion Day Care Centre Mkoani Geita.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Bw. Daniel Patrick Kapaya, ametoa wito kwa wazazi wa mikoa sita ya Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao hasa wanapokuwa wakitumia mitandao ya kijamii.

Bw. Kapaya ametoa wito huo akiwa mgeni rasmi katika sherehe ya shule ya awali ya Marion Day Care Centre, iliyopo Mji wa Katoro, mkoani Geita ambapo Sherehe hiyo ilihudhuriwa na watoto pamoja na wazazi, na kwamba Katibu huyo amesisitiza umuhimu wa kuwalinda watoto dhidi ya athari za mitandao ya kijamii.

"Kwa kizazi hiki, watoto wanatumia muda mwingi mtandaoni kupitia simu, kishikwambi, YouTube, na Smart TVs, kiasi cha kutumia takriban masaa 8 kwa siku. Ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha watoto wanatumia mitandao hii kwa manufaa bora badala ya kuwa katika hatari ya ukatili mtandaoni," amesema Kapaya.

Aidha, Katibu huyo amehimiza wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni kwa kuhakikisha wanafanya kazi za nyumbani (homework) na kukagua madaftari yao mara kwa mara.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa shule hiyo, Bi. Domitila Francis, ameungana na Katibu huyo kwa kusisitiza umuhimu wa wazazi kutambua majukumu yao katika malezi ya watoto na kupambana na ukatili wa aina yoyote.

Sherehe hiyo imeacha somo muhimu kwa wazazi kuhusu jukumu lao la kuhakikisha usalama wa watoto mtandaoni na kuweka kipaumbele katika malezi bora ya watoto.

Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Bw. Daniel Patrick Kapaya, akizungumza kwenye mahafali hayo katika shule ya awali Marion Day Care Centre Mkoani Geita.



 

Previous Post Next Post