KATIBU WA SMAUJATA KANDA YA ZIWA DANIEL KAPAYA APONGEZA HARAKATI ZA KUPINGA UKATILI MWAKA 2024

Na Mapuli Kitina Misalaba
 
Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, leo tarehe 31 Desemba 2024, akiwa katika ofisi za SMAUJATA, ametoa tathmini ya mafanikio ya harakati za kupinga vitendo vya kikatili kwa mwaka 2024.

Bwana Kapaya amesema viongozi wa SMAUJATA katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa wameonyesha juhudi kubwa katika kuibua na kupinga vitendo vya kikatili kwa kushirikiana na vyombo vya habari na jamii. 

Kupitia matamko mbalimbali, SMAUJATA imeongeza uelewa wa jamii juu ya kuripoti matukio kwa vyombo vya dola, ikiwa ni pamoja na matumizi ya simu ya dharura 116.

Kwa kushirikiana na dawati la jinsia, ustawi wa jamii, na maendeleo ya jamii, SMAUJATA imefanikiwa kupambana na wahalifu na kuendeleza umoja wa viongozi wake. 

Bwana Kapaya amesema ikiwa ushirikiano huo utaendelea mwaka 2025, kuna matumaini makubwa ya kupunguza matukio ya uhalifu kama ubakaji, ulawiti, ukeketaji, rushwa, madawa ya kulevya, mirathi, ardhi, na mimba za utotoni.

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa imebaki kuwa ucheleweshwaji wa maamuzi ya kesi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Bwana Kapaya ameziomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha mashauri ya mirathi, hususani kwa wajane na wagane, yanashughulikiwa kwa wakati ili kuepusha mlundikano wa majalada.

Katibu pia ameomba ushirikiano zaidi kati ya viongozi na vyombo vya sheria ili kuhakikisha kesi zote za ukatili zinafikishwa mahakamani na haki kutolewa kwa wakati.

Bwana Kapaya amewataka viongozi wa SMAUJATA kutokata tamaa katika mapambano dhidi ya makundi ya watu waovu, huku akiwahimiza kuwa na utulivu katika kipindi hiki cha mwala mpya. 

Amehitimisha kwa kuwatakia wananchi wa Kanda ya Ziwa (Shinyanga, Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu na Mara) heri ya mwaka mpya 2025 wenye mafanikio katika vita dhidi ya ukatili na uhalifu.

Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) ni jumuiya ya kupinga ukatili nchini ambayo inatekeleza majukumu yake chini ya Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum


Previous Post Next Post