Maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza kufuatilia
Ligi ya Krismas CUP inayoendelea katika Uwanja wa Mhangu, Kata ya Salawe,
Wilaya ya Shinyanga vijijini.
Mashindano haya yameandaliwa na Makamba Lameck
kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka, kwa lengo la kuibua
vipaji vya michezo mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani.
Ligi hiyo inajumuisha jumla ya timu 16, ambapo leo
imechezwa mechi ya saba kati ya Mwagiligili FC na Mahando FC, timu zote kutoka
Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.
Katika mchuano huo, Mahando FC wameibuka washindi
kwa ushindi wa mabao 3-2 ambapo wafungaji wa Mahando FC ni Ramadhan Vita
aliyepachika mabao mawili na Hamis Hamis aliyekamilisha ushindi, huku
Mwagiligili FC wakijibu kupitia mabao ya Thomas Mula na Miyco Michal.
Awali, kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kwa
wasichana wa Sekondari ya Mhangu dhidi ya Salawe, ambapo dakika 90 za kawaida
zilimalizika kwa sare ya 1-1. Hatimaye, Mhangu Girls waliibuka washindi kwa
mikwaju ya penati 3-2 na kutwaa zawadi yao.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock
Kijida, amesema mashindano hayo yanaendelea vizuri huku wachezaji wakionesha
nidhamu ya hali ya juu ambapo ameendelea kuhimiza wananchi, viongozi, na wadau
wa michezo kujitokeza kwa wingi kufuatilia mechi hizo.
Mwalimu Kijida amebainisha kuwa kesho kutakuwa na
mechi ya nane, kati ya Modern FC na Mwasenge FC, ambayo itahitimisha hatua ya
mtoano kabla ya kuingia kwenye robo fainali.
Baadhi ya viongozi ambao wamehudhuria mashindano
hayo wameendelea kumpongeza Makamba Lameck kwa kuandaa ligi hiyo inayowavutia
wananchi kwa kiingilio cha bure, tofauti na mashindano mengine.
Mashindano haya yanatarajiwa kufikia kilele chake
Disemba 17, 2024.
Endelea
kufuatilia ligi hii kupitia mitandao yetu ya kijamii kwa jina la MISALABA
MEDIA.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock
Kijida, akizungumza.
Makamba Lameck mdau wa Michezo ndiye mwandaaji na mdhamini wa ligi ya Krismas CUP kupitia kampuni yake ya MCL, inayojihusisha na biashara ya nafaka.