MAHAFARI YA NNE YA SUNRISE NURSERY AND DAY CARE YAFANA, JAMII YATAKIWA KUWAJIBIKA KWA MALEZI YA WATOTO

Mkurugenzi wa kituo cha kituo cha kulea watoto cha Sunrise Nursery and Day Care, Mwalimu Ndaki Mathias, akizungumza kwenye mahafali hayo ya nne 2024.

Na Elisha Petro, Misalaba Media

Mahafari ya nne ya kituo cha kulea watoto cha Sunrise Nursery and Day Care kilichopo Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, yamefanyika leo Jumamosi, tarehe 7 Desemba 2024, katika ukumbi wa kituo hicho ambapo Wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla wametakiwa kuwajibika kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto ili kuwaepusha na mambo hatarishi kama ukatili wa kijinsia na utekaji.

Katika mahafali hayo, mgeni rasmi ni Simon Maximilian Kadogosa, Msimamizi wa Utafiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (Monitoring and Evaluation Specialist, Tanzania Red Cross Society). 

Katika hotuba yake, Kadogosa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, walezi, na wamiliki wa kituo hicho katika kuhakikisha watoto wanalelewa kwa maadili mema na kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote.

“Katika jamii yetu tumekuwa tukishuhudia matukio ya ukatili yanayowalenga watoto, lakini ukatili huu unatokea ndani ya jamii zetu. Niwaombe wanajamii wote tushirikiane na kituo hiki kwa kuhamasishana kuleta watoto hapa. Jukumu la kumlea mtoto ni la jamii nzima, si kwa mzazi peke yake au mwalimu tu. Serikali inajitahidi, lakini juhudi zake zinahitaji mshikamano wetu sote. Tukiwalinda watoto, tunalinda taifa na kutengeneza ustawi stahimikivu kupitia watoto hao,” amesema Kadogosa.

Kadogosa pia amekemea matukio ya utekaji na ulawiti wa watoto, akihimiza jamii kushirikiana katika kulinda ustawi wa watoto kwa lengo la kuandaa kizazi bora chenye maadili.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kitangili, Mhe. Mariam Nyangaka, amepongeza uongozi wa kituo cha Sunrise Nursery and Day Care kwa juhudi kubwa wanazofanya katika malezi ya watoto.

“Kwanza niwapongeze viongozi na watumishi wa kituo hiki kwa kazi kubwa mnayoifanya. Niwaombe muendelee kuweka mazingira wezeshi zaidi ya kuwalea na kuwatunza watoto wetu. Kituo hiki ni bora sana kwa hapa Kitangili, na kinatoa mchango mkubwa kwa jamii yetu,” amesema Diwani Nyangaka.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Mwalimu Ndaki Mathias, amewashukuru wazazi na walezi kwa kuendelea kuwaamini na kuwapeleka watoto wao kituoni hapo.

“Kwanza niwashukuru kwa kuendelea kutuamini na kuleta watoto hapa kwetu. Ninawahakikishia usalama wa watoto wenu na elimu bora. Tukishirikiana kwa weledi, hekima, na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tunaweza kufika mbali zaidi. Watoto wanahitaji malezi na matunzo ili waweze kufanikisha ndoto zao,” amesema Mwalimu Ndaki.

Aidha, wazazi na walezi waliohudhuria mahafali hayo wameeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa na kituo hicho, wakibainisha kuwa malezi na elimu inayotolewa inawasaidia watoto kuongeza uwezo wa kufikiri, kulinda maadili mema, na kuwaandaa vyema kujiunga na shule za msingi.

Kwa mwaka huu wa 2024, jumla ya watoto 78 wamesajiliwa katika kituo hicho, ambapo wanafunzi 24 wamehitimu masomo yao ya awali. Mahafali hayo yamehitimishwa kwa burudani mbalimbali kutoka kwa watoto, ikiwa ni pamoja na nyimbo, michezo ya kuigiza, na ngonjera zilizosisitiza umuhimu wa elimu na maadili mema.

Sunrise Nursery and Day Care imeendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwajenga watoto kwa misingi ya kiroho, kijamii, na kielimu, ikiwavutia wazazi kutoka maeneo mbalimbali ya Kitangili na nje ya Shinyanga.

Mgeni rasmi katika mahafali ya nne ya kituo cha watoto Sunrise Nursery and Day Care, Msimamizi wa Utafiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (Monitoring and Evaluation Specialist, Tanzania Red Cross Society) Simon Maximilian Kadogosa, akizungumza leo Desemba 7, 2024.

Diwani wa Kata ya Kitangili, Mhe. Mariam Nyangaka, akizungumza kwenye mahafali ya nne ya kituo cha watoto Sunrise Nursery and Day Care leo Desemba 7, 2024.



Previous Post Next Post