Makamba Mussa Lameck, mdau wa Michezo ambaye ndiye mwandaaji na mdhamini wa Krismas CUP.
Na
Mapuli Kitina Misalaba
Ligi ya Krismas CUP, iliyoandaliwa na kudhaminiwa na Bwana Makamba Mussa
Lameck, imeleta msisimko mkubwa kwa wapenzi wa michezo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Ligi hiyo ilianza rasmi tarehe 28
Desemba 2024 baada ya kupokea kibali kutoka SHIREFA ya mkoa na wilaya, ikiwa na
lengo la kutoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao na kuchangia maendeleo ya
jamii kupitia michezo.
MUUNDO
WA LIGI
Ligi hiyo ilijumuisha jumla ya timu
16, zikiwemo:
Kano FC, Mahembe FC, Sec Combine FC,
Isenengeja FC, Machongo FC, Mwabenda FC, Salawe FC, Solwa FC, Beya FC, Ngubalu
FC, Ikonongo FC, Mwawile FC, Mwagiligili FC, Mahando FC, Modern FC, na Mwasenge
FC.
- Timu 7 kutoka kata ya Salawe
- Timu 4 kutoka kata jirani za Solwa, Mwenge, na
Mwakitolyo
- Timu 5 kutoka Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.
Mashindano yalianza kwa mechi za
mtoano, ambapo kila timu ilicheza mechi moja, na timu 8 zilizoibuka washindi
ziliingia hatua ya robo fainali ambapo hatua hiyo ilifuatwa na nusu fainali na
hatimaye mechi ya fainali iliyofanyika tarehe 19 Desemba 2024.
Kwa jumla, michezo 16 ilichezwa na
zaidi ya wachezaji 250 walishiriki, ambapo mabao 29 yalifungwa, kadi 31 za
njano zilitolewa, na kadi nyekundu 4.
WACHEZAJI
WALIOCHAGULIWA KUUNDA TIMU YA PAMOJA
Ili kuhakikisha vipaji
vilivyooneshwa vinapewa nafasi zaidi, wachezaji 50 walichaguliwa kuunda timu ya
pamoja (combine team) ambapo timu hiyo itafanya mazoezi na kushiriki mashindano
mbalimbali yakiwemo ya mkoa mwakani lakini pia, makocha wa timu hii walipewa
jukumu la kuandaa ratiba ya mazoezi na kuhakikisha wachezaji hawa wanapata
mafunzo bora.
ZAWADI
NA UTAMBUZI
Kwa kusherehekea mafanikio ya ligi,
zawadi mbalimbali zilitolewa:
- Mshindi wa kwanza:
Tuzo ya shilingi 1,000,000.
- Mshindi wa pili:
Tuzo ya shilingi 500,000.
- Mshindi wa tatu:
Tuzo ya shilingi 200,000.
- Zawadi binafsi
kwa mchezaji bora, golikipa bora, na mfungaji bora, kila mmoja akipewa
shilingi 50,000.
- Timu yenye nidhamu ilipata seti moja ya jezi.
MECHI
ZA WANAWAKE
Kama sehemu ya kuhamasisha ushiriki
wa wanawake katika michezo, mechi moja ilichezwa kati ya timu za Mhangu
Secondary Girls na Salawe Secondary Girls ambapo Mhangu Girls walishinda kwa
njia ya penati na kutunukiwa zawadi ya shilingi 50,000 na kwamba tukio hilo
liliibua hamasa kubwa na kuvutia mashabiki wengi wa michezo wa jinsia zote.
CHANGAMOTO
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu
Emmanuel Enock Kijida alisema pamoja na mafanikio, changamoto zifuatazo
zilijitokeza:
1.
Nidhamu mbovu kwa baadhi ya
wachezaji na mashabiki.
2.
Gharama kubwa za kupata vibali vya
uendeshaji wa ligi.
3.
Mitazamo potofu ya kisiasa
inayochukulia juhudi za michezo kama nia za kisiasa.
4.
Miundombinu duni ya viwanja.
5.
Vurugu zisizo na sababu kutoka kwa
mashabiki na viongozi wa timu.
MAPENDEKEZO
Kamati ya ligi imependekeza hatua
mbalimbali za kuboresha ligi zijazo:
- Mafunzo kwa waamuzi ili kuhakikisha wanazingatia sheria
za mpira kwa usahihi.
- Kupunguza gharama za vibali vya kuendesha ligi ili
kuvutia wadau zaidi.
- Kuweka msisitizo wa kutoshirikisha siasa katika masuala
ya michezo.
Makamba Mussa Lameck aliahidi kuendelea kuandaa ligi
za michezo kila mwaka ambapo alisema siyo mara yake ya kwanza kuandaa ligi ya michezo
kwani amekuwa akiandaa ligi za ndondo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa
Geita na kwamba sasa ameamua kuandaa ligi pia kwenye Wilaya ya Shinyanga
Vijijini ili kuibua vipaji vya michezo miongoni mwa vijana wa Mkoa wa
Shinyanga.
Hadi sasa, jumla ya wachezaji 50 wamechaguliwa kama
sehemu ya ajira yao.
Ligi hiyo, ilivutia maelfu ya wananchi waliojitokeza kufuatilia mechi
mbalimbali kwa hamasa kubwa huku wakimshukuru na kumpongeza Makamba Mussa
Lameck kwa kuandaa liyo.
HITIMISHO
Ligi ya Krismas CUP imefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kutokana na juhudi za mdhamini Bwana Makamba Mussa Lameck, viongozi
wa serikali, na mashabiki ambapo Bwana
Makamba ametoa mchango mkubwa wa kifedha kufanikisha mashindano hayo na kwamba
gharama za uendeshaji zilikadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni saba.
Mwalimu Emmanuel Enock Kijida “kwa
niaba ya kamati ya ligi, tunatoa shukrani za pekee kwa mdhamini, waamuzi,
vyombo vya habari kama MISALABA MEDIA, na kamati ya ulinzi na usalama kwa
kuhakikisha mashindano haya yamefanikiwa”.
Ligi hii imedhihirisha kuwa michezo
ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha watu, kukuza vipaji, na kuchangia maendeleo
ya jamii wakati huo huo wito unatolewa kwa wadau wote kuendelea kushirikiana
ili kufanikisha malengo haya ya kuinua vipaji na kufanikisha mashindano bora
zaidi siku za usoni.
MISALABA
MEDIA inatoa shukrani za dhati kwa Makamba Mussa Lameck pamoja na kamati yake
kwa kutuamini na kutupatia nafasi ya kuripoti taarifa zote za ligi hiyo na
kwamba tunaahidi kuwa, endapo tutapata nafasi tena katika awamu zijazo,
tutafanya kazi kwa ubunifu zaidi na kuhakikisha tunatoa taarifa bora
zinazokidhi matarajio ya wadau wa michezo.