WACHEZAJI 50 WAPATA AJIRA AWAMU YA KWANZA KATIKA LIGI INAYODHAMINIWA NA MAKAMBA MUSSA LAMECK

  

Makamba Mussa Lameck, mdau wa Michezo ambaye ndiye mwandaaji na mdhamini wa Krismas CUP.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Ligi ya Krismas CUP,  iliyoandaliwa na kudhaminiwa na Bwana Makamba  Mussa  Lameck, imeleta msisimko mkubwa kwa wapenzi wa michezo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Ligi hiyo ilianza rasmi tarehe 28 Desemba 2024 baada ya kupokea kibali kutoka SHIREFA ya mkoa na wilaya, ikiwa na lengo la kutoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia michezo.

MUUNDO WA LIGI

Ligi hiyo ilijumuisha jumla ya timu 16, zikiwemo:

Kano FC, Mahembe FC, Sec Combine FC, Isenengeja FC, Machongo FC, Mwabenda FC, Salawe FC, Solwa FC, Beya FC, Ngubalu FC, Ikonongo FC, Mwawile FC, Mwagiligili FC, Mahando FC, Modern FC, na Mwasenge FC.

  • Timu 7 kutoka kata ya Salawe
  • Timu 4 kutoka kata jirani za Solwa, Mwenge, na Mwakitolyo
  • Timu 5 kutoka Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.

Mashindano yalianza kwa mechi za mtoano, ambapo kila timu ilicheza mechi moja, na timu 8 zilizoibuka washindi ziliingia hatua ya robo fainali ambapo hatua hiyo ilifuatwa na nusu fainali na hatimaye mechi ya fainali iliyofanyika tarehe 19 Desemba 2024.

Kwa jumla, michezo 16 ilichezwa na zaidi ya wachezaji 250 walishiriki, ambapo mabao 29 yalifungwa, kadi 31 za njano zilitolewa, na kadi nyekundu 4.

WACHEZAJI WALIOCHAGULIWA KUUNDA TIMU YA PAMOJA

Ili kuhakikisha vipaji vilivyooneshwa vinapewa nafasi zaidi, wachezaji 50 walichaguliwa kuunda timu ya pamoja (combine team) ambapo timu hiyo itafanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali yakiwemo ya mkoa mwakani lakini pia, makocha wa timu hii walipewa jukumu la kuandaa ratiba ya mazoezi na kuhakikisha wachezaji hawa wanapata mafunzo bora.

ZAWADI NA UTAMBUZI

Kwa kusherehekea mafanikio ya ligi, zawadi mbalimbali zilitolewa:

  • Mshindi wa kwanza: Tuzo ya shilingi 1,000,000.
  • Mshindi wa pili: Tuzo ya shilingi 500,000.
  • Mshindi wa tatu: Tuzo ya shilingi 200,000.
  • Zawadi binafsi kwa mchezaji bora, golikipa bora, na mfungaji bora, kila mmoja akipewa shilingi 50,000.
  • Timu yenye nidhamu ilipata seti moja ya jezi.

MECHI ZA WANAWAKE

Kama sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika michezo, mechi moja ilichezwa kati ya timu za Mhangu Secondary Girls na Salawe Secondary Girls ambapo Mhangu Girls walishinda kwa njia ya penati na kutunukiwa zawadi ya shilingi 50,000 na kwamba tukio hilo liliibua hamasa kubwa na kuvutia mashabiki wengi wa michezo wa jinsia zote.

CHANGAMOTO

Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida alisema pamoja na mafanikio, changamoto zifuatazo zilijitokeza:

1.    Nidhamu mbovu kwa baadhi ya wachezaji na mashabiki.

2.    Gharama kubwa za kupata vibali vya uendeshaji wa ligi.

3.    Mitazamo potofu ya kisiasa inayochukulia juhudi za michezo kama nia za kisiasa.

4.    Miundombinu duni ya viwanja.

5.    Vurugu zisizo na sababu kutoka kwa mashabiki na viongozi wa timu.

MAPENDEKEZO

Kamati ya ligi imependekeza hatua mbalimbali za kuboresha ligi zijazo:

  • Mafunzo kwa waamuzi ili kuhakikisha wanazingatia sheria za mpira kwa usahihi.
  • Kupunguza gharama za vibali vya kuendesha ligi ili kuvutia wadau zaidi.
  • Kuweka msisitizo wa kutoshirikisha siasa katika masuala ya michezo.

Makamba Mussa Lameck aliahidi kuendelea kuandaa ligi za michezo kila mwaka ambapo alisema siyo mara yake ya kwanza kuandaa ligi ya michezo kwani amekuwa akiandaa ligi za ndondo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Geita na kwamba sasa ameamua kuandaa ligi pia kwenye Wilaya ya Shinyanga Vijijini ili kuibua vipaji vya michezo miongoni mwa vijana wa Mkoa wa Shinyanga.

Hadi sasa, jumla ya wachezaji 50 wamechaguliwa kama sehemu ya ajira yao.
Ligi hiyo, ilivutia maelfu ya wananchi waliojitokeza kufuatilia mechi mbalimbali kwa hamasa kubwa huku wakimshukuru na kumpongeza Makamba Mussa Lameck kwa kuandaa liyo.

HITIMISHO

Ligi ya Krismas CUP imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za mdhamini Bwana Makamba Mussa Lameck, viongozi wa serikali, na mashabiki ambapo  Bwana Makamba ametoa mchango mkubwa wa kifedha kufanikisha mashindano hayo na kwamba gharama za uendeshaji zilikadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni saba.

Mwalimu Emmanuel Enock Kijida “kwa niaba ya kamati ya ligi, tunatoa shukrani za pekee kwa mdhamini, waamuzi, vyombo vya habari kama MISALABA MEDIA, na kamati ya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha mashindano haya yamefanikiwa”.

Ligi hii imedhihirisha kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha watu, kukuza vipaji, na kuchangia maendeleo ya jamii wakati huo huo wito unatolewa kwa wadau wote kuendelea kushirikiana ili kufanikisha malengo haya ya kuinua vipaji na kufanikisha mashindano bora zaidi siku za usoni.

MISALABA MEDIA inatoa shukrani za dhati kwa Makamba Mussa Lameck pamoja na kamati yake kwa kutuamini na kutupatia nafasi ya kuripoti taarifa zote za ligi hiyo na kwamba tunaahidi kuwa, endapo tutapata nafasi tena katika awamu zijazo, tutafanya kazi kwa ubunifu zaidi na kuhakikisha tunatoa taarifa bora zinazokidhi matarajio ya wadau wa michezo.

Makamba Mussa Lameck, mdau wa Michezo ambaye ndiye mwandaaji na mdhamini wa Krismas CUP.Makamba Mussa Lameck, mdau wa Michezo ambaye ndiye mwandaaji na mdhamini wa Krismas CUP.
Previous Post Next Post