Na.
Faraja Mbise, DDODOMA
Wananchi
wameshauriwa kushiriki katika kila hatua ya maendeleo ya nchi ili kuimarisha
demokrasia kwasababu wanaposhiriki katika maendeleo wanapata fursa ya kuibua
changamoto na fursa zilizopo sambamba na kueleza mawazo yao na kutoa
mapendekezo.
Hayo,
yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akizungumza
na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mdahalo wa Miaka 63 ya Uhuru wa
Tanzania Bara, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. “Ndugu zangu, sisi kwenye serikali, kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hata kwenye hatua ya kuweka
miongozo, tunawajibika sana kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika hatua
zote za kujiletea maendeleo. Viongozi mtakubaliana na mimi hata wakati wa
kupigania uhuru viongozi hawa mashuhuri tunaowasema hawakuwa pekeyao. Hata leo
kuleta maendeleo ya Tanzania hatuwezi kuwa na viongozi pasipo kuwashirikisha
wananchi. Wananchi wanashirikishwa sana katika maeneo yao, kwanza kwenye kuibua
vipaumbele vya maendeleo” alisema Alhaj Shekimweri.
Alitoa
pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kwa kupiga hatua kubwa ya
maendeleo tangu Tanzania bara ilipopata uhuru wake mpaka hivi sasa. “Natoa
pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, kwa kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wetu na kuendeleza mambo mengi sana
ya maendeleo yenye tija kwa nchi yetu. Pia kujenga diplomasia na mahusiano ya
kimataifa na mataifa mengine katika namna ambayo pia inaendelea kunufaisha nchi
yetu. Tunamtia nguvu katika kila changamoto anayopitia kama kiongozi, najua
mahitaji ya watanzania ni makubwa, najua kuna vita kubwa ya kiuchumi na
kimaadili. Lakini kwa hakika watanzania tunatambua kwamba, nchi yetu miaka 63
baada ya Uhuru, imepiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo na kwamba ipo katika
uelekeo mkubwa zaidi wa kufanya maendeleo makubwa zaidi” alipongeza Alhaj
Shekimweri.
Kuhusu
mila, tamaduni na jadi zetu, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma aliwaasa wananchi
kuzienzi na kutunza mila na tamaduni zetu. “Maana ya kuwa huru, ni kuwa na
taifa lenye utambulisho wake wa mila, desturi na tamaduni zake. Na tunamuenzi Mwalimu
Nyerere, hapo aliwahi kusema, ‘asiyejali mila zake ni mtumwa’. Sisi
watanzania tuna tamaduni nzuri sana, mila nzuri sana, jadi nzuri sana na
tunazienzi, zitambua na kuzithamini” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa
upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliwataka
wananchi kulinda Uhuru wa Tanzania kwa kufanya kazi ili waweze kujitegemea
kiuchumi na kuwasisitiza kuwa, hiyo ndio maana halisi ya kuwa na uhuru. “Hakuna
uhuru wa taifa kama hakuna uhuru binafsi, hatuwezi kuulinda uhuru wa taifa kama
hatuwezi kulinda uhuru wetu binafsi, tujikomboe kifikra, kiuchumi ndipo
tunaweza kuikomboa nchi kama taifa. Kwahiyo, tujiimarishe sana kuhakikisha
kwamba tunalinda uhuru wetu. Mwalimu Nyerere wakati ule ilikuwa Uhuru na Kazi,
baadae tulipogndua kuwa kazi ni muhimu tukasema uhuru ni kazi, hapa falsafa
maana yake ni nini: hatuwezi kusema tumejikomboa tuko huru kama hatufanyi kazi,
lakini hapa inatukumbusha wazi kwamba, uhuru wetu utakuwa na maana pale
tutakapokuwa na uwezo wa kujitegemea na utajitegemeaje ni kwa kufanya kazi kwa
bidii” alisisitiza Prof. Mwamfupe.
Nae
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alizungumzia maendeleo ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) jinsi yalivyorahisisha suala la
mawasiliano katika utendaji kazi ukilinganisha na kipindi cha nyuma wakati wa
kupambania Uhuru wa Tanzania bara. “Miongoni mwa vitu ambavyo nchi yetu imepiga
maendeleo makubwa sana ni kwenye teknolojia kwa maana ya matumizi ya TEHAMA. Zamani
ilikuwa unapotaka kusafiri lazima ufike stendi ukakate tiketi lakini sasahivi,
huna haja ya kwenda stendi, unaweza ukafanya hivyo ukiwa nyumbani kwako. Zamani
ilikuwa kama unataka kutoa au kuweka hela benki lazima uende kwenye benki na
ukapange foleni, lakini siku hizi unaweza kufanya miamala kwenye simu na kwa
mawakala ni kwasababu ya matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano. Na kwenye eneo hilo la mikopo ya asilimia 10 unajisajili kwenye
mfumo huna haja ya kuja ofisini. Kwahiyo, matumizi ya teknolojia tunaona jinsi
ambavyo yamekua na sisi kama Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunaendelea kutumia
hiyo mifumo” alisema Fungo kwa ujasiri mkubwa.
Akizungumzia
masuala ya mmomonyoko wa maadili, Mwanasheria wa Baraza la Machifu Mkoa wa Dodoma,
Samwel Chimanyi aliwataka wananchi hasa vijana kuachana na makundi ambayo yanaathiri
mifumo ya maadili ya kitanzania. “Hili eneo mkalitafsiri vizuri nyie mlioko
shuleni, tuachane na kuiga makundi ambayo yamejielekeza kwenye tabia zinazoathiri
mifumo ya maadili yetu. Kwahiyo, watemi wanaendelea kutoa rai na kulaani vikali
masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na vitu vinavyoendelea ambayo sio vizuri kwa
maadili ya kitanzania” alitoa rai Chimanyi.
Kuimarika
kwa ushirikishwaji wa wananchi kutokana na mfumo wa kidemokrasia wa vyama
vingi, mchangiaji wa mada kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nasma Ally
alizungumzia kuhusu ushirikishwaji wa wanawake katika kuwania nafasi mbalimbali
za uongozi. “Kupitia mfumo wa vyama vingi, ushirikishwaji wa wananchi pamoja na
mkusanyo wa mawazo katika taifa letu uliimarika. Sambamba na hilo Serikali ya
Tanzania iliweza kuanzisha Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo inasimamia uchaguzi
wa huru na haki. Demokrasia ni haki na usawa, kwakuzingatia hilo pia, Serikali
ya Tanzania iliweza kuongeza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi.
Hii ilifanyika pale Tanzania ilipoongeza siti maalumu kwa wanawake. Takwimu
zinasema kutoka mwaka 1990 asilimia 4.6 zilikuwa ni kwa ajili ya wanawake
Bungeni za viti maalum, kwa mwaka 2020 asilimia 36.6 ni siti maalum za wanawake.
Tunapoona wanawake wanashiriki katika masuala ya nchi, hii inonesha kwamba
jamii pamoja na serikali mwanamke ni kiongozi wa familia, jamii na ana mchango
mkubwa sana katika kuilea jamii na kupelekea maendeleo ya taifa” alisema Ally.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Dodoma, Fatuma Madidi alichangia mada
kwa kugusia maendeleo ya miundombinu katika sekta ya usafirishaji na elimu kwa
kuipongeza serikali kwa kujikita katika maendeleo tangu ulipopatikana uhuru wa
Tanzania bara. “Ile dhana ya Baba wa Taifa ya kufuta ujinga imekamilika na
kwamba sasa kila mmoja ana haki ya kwenda shule na kusoma. Katika swala la
miundombinu utaona kwamba, sasahivi barabara nyingi zinaingilika na na
zinapitika na hakuna hata ule muingiliano baina ya wilaya na wilaya, na mkoa
kwa mkoa. Sasahivi lile tatizo la usafiri limekuwa ni historia” alichangia
Madidi.
Tanzania
bara huadhimisha uhuru wake ifikapo Desemba 09 ya kila mwaka na kaulimbiu ya
maadhimisho hayo ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ni “Uongozi
Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo yetu”.
MWISHO