MILIONI 407 ZATUMIKA KUSAMBAZA MAJIKO YA GESI KILIMANJARO


 Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatarajia kusambaza jumla ya majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita 19,530 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 katika mkoa wa Kilimanjaro. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024-2034.


Akizungumza Novemba 6, 2024, Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi wa REA, Mhandisi Emanuel Yesaya, alisema mradi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata majiko kwa bei nafuu. Alitoa taarifa hiyo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa kutambulisha mradi huo pamoja na msambazaji wa majiko, Kampuni ya Lake Gas.

“Tumeanza rasmi utekelezaji wa mradi huu ambao unagharimu shilingi milioni 407 kwa mkoa wa Kilimanjaro. Kampuni ya Lake Gas itahusika na usambazaji wa majiko haya kwa wananchi,” alisema Mhandisi Yesaya.

Alifafanua kuwa, mradi huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia badala ya kuni na mkaa.



Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Katibu Tawala wa Mkoa, Kiseo Nzowa, aliipongeza REA kwa juhudi zake za kutekeleza ajenda ya Rais Samia ya matumizi ya nishati safi.

“Tunahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hii ya majiko ya gesi yenye ruzuku, kwani matumizi ya nishati safi yanalinda mazingira, kuboresha afya na kuokoa muda wa kufanya shughuli za kiuchumi,” alisema Nzowa.


Kwa mujibu wa Mhandisi Yesaya, mwaka wa fedha 2024/2025 utashuhudia usambazaji wa majiko ya gesi 452,445 yenye thamani ya shilingi bilioni 10 kote nchini kwa ruzuku ya asilimia 50. Aidha, REA pia inaandaa mradi wa usambazaji wa majiko banifu 200,000 kwa ruzuku ya asilimia 75 hadi 85 kwa wakazi wa vijijini.

Hatua hii inalenga kuhakikisha Watanzania wa kipato cha chini wanafikiwa, na kufanikisha lengo la kufikia asilimia 80 ya wananchi wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Previous Post Next Post