Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, anatarajiwa kufanya ziara ya kijiji kwa kijiji katika Tarafa ya Samuye kuanzia Desemba 18 hadi Desemba 24, 2024. Ziara hiyo imelenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Mtatiro atatembelea vijiji 15 vilivyopo katika Kata za Usanda, Samuye, Mwamala, na Masengwa. Kila kijiji kitapata muda maalum wa kuwasilisha changamoto zinazowakumba, huku viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya wakishiriki katika jitihada za kuzipatia ufumbuzi.
Ratiba ya Ziara:
Desemba 18, 2024: Vijiji vya Shabuluba, Ngangalulwa, na Nzagaluba (Kata ya Usanda).
Desemba 19, 2024: Vijiji vya Singita, Manyada (Kata ya Usanda) na Mwang’halanga (Kata ya Samuye).
Desemba 20, 2024: Vijiji vya Isela, Ibingo, na Idodoma (Kata ya Samuye).
Desemba 21, 2024: Vijiji vya Ishinabulandi, Bunonga, na Mwamala (Kata ya Mwamala).
Desemba 23, 2024: Vijiji vya Ibanza, Bugogo, na Ikonda (Kata ya Mwamala).
Desemba 24, 2024: Vijiji vya Masengwa, Ilobashi, na Bubale (Kata ya Masengwa).
Ziara hizi zinaanza asubuhi saa 4:00 na kumalizika mchana au jioni, kutegemea na idadi ya kero na mahitaji ya kijiji husika.
Mkuu wa Wilaya, Wakili Mtatiro, amesisitiza kuwa lengo kuu la ziara hii ni kuimarisha mahusiano kati ya serikali na wananchi, huku akitilia mkazo umuhimu wa kutoa majibu ya haraka kwa changamoto zinazowakabili wananchi wa Tarafa ya Samuye.
Wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika mikutano hiyo ili kutoa maoni na kueleza matatizo yao moja kwa moja kwa kiongozi huyo wa wilaya.