Na Mapuli Kitina Misalaba
Msimamizi wa ligi ya Krismas Cup, Mwalimu Emmanuel,
ametoa wito kwa taasisi za michezo na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi
kushuhudia vipaji vya vijana katika mashindano yanayoendelea kata ya Salawe,
Wilaya ya Shinyanga Vijijini.
Akizungumza na Misalaba Media, Mwalimu Emmanuel
amesema mashindano hayo yameleta burudani na fursa kubwa ya kugundua vipaji
vipya ambapo leo, ligi hiyo itaendelea kwa mechi kati ya Mwagiligili FC na Mahando
FC, timu zote kutoka Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza na kwamba kabla ya
mechi hiyo, kutakuwa na burudani ya mchezo wa mpira wa miguu kwa wasichana
kutoka Shule za Sekondari za Mhangu na Salawe ambapo mshindi atapewa zawadi.
“Tumeamua
kuibua vipaji kwa upande wa wasichana kwa sababu tunaamini hata wao wanaweza
kung'ara katika mpira wa miguu. Mfano ni timu za ligi kuu za wanawake kama
Simba Queens na Yanga Princess. Lengo ni kuhakikisha vipaji hivi vinapata
nafasi ya kuonekana na kukuza soka kwa wanawake,”
amesema Mwalimu Emmanuel.
Mashindano hayo yamedhaminiwa na Makamba Lameck
kupitia kampuni yake ya MCL, inayojihusisha na biashara ya nafaka, kwa lengo la
kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo mkoani Shinyanga.
Aidha, Mwalimu Emmanuel amepongeza nidhamu ya timu
zinazoshiriki na kutoa wito kwa viongozi wa soka, wakiwemo wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Shirikisho la Mpira wa Miguu Shinyanga
(SHIREFA), na wadau wengine wa michezo, kufika kushuhudia na kusaidia kukuza
vipaji.
“Mpaka
sasa tumeshachagua wachezaji 22 kwa scauting, na mashindano haya yamekuwa na
mafanikio makubwa. Robo fainali itaanza rasmi Jumamosi ijayo, huku mechi za
awali zikitarajiwa kumalizika Ijumaa. Siku ya Jumapili tutakuwa na mapumziko
kabla ya kuendelea na hatua za mwisho,” amesema Mwalimu Kijida
Ligi hiyo inashirikisha jumla ya timu 16, zikiwemo
timu kutoka Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza.
Mashindano ya Krismas Cup yanatarajiwa kufikia
kilele chake tarehe 17 Desemba 2024, yakibeba matumaini ya vijana wengi
wanaotafuta nafasi ya kung'ara kwenye medani ya michezo kitaifa na kimataifa.
Timu za michezo ikiwemo ligi kuu, ligi daraja la kwanza na wadau mbalimbali wa michezo wametakiwa kuchangamkia fursa za kuwatambua na kuwaendeleza wachezaji hawa wachanga kwa manufaa ya taifa.
Makamba Lameck mdau wa Michezo ndiye mwandaaji na mdhamini wa ligi ya Krismas CUP kupitia kampuni yake ya MCL, inayojihusisha na biashara ya nafaka.
TAZAMA VIDEO SHULE YA MHANGU WAKIZUNGUMZA JANA.