Na Mapuli Kitina Misalaba
Kamweji Tungu Kapela, mkazi wa Nhelehani, kata ya
Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, ameieleza MISALABA MEDIA kuwa mtoto wake mwenye
umri wa miaka minne alipatwa na tukio la kuogofya baada ya kung’atwa kichwani
na fisi mnamo Novemba 28, 2024, hali iliyosababisha kuathiri afya ya mtoto huyo.
Akisimulia tukio hilo, Kapela amesema lilitokea
majira ya saa kumi na mbili jioni wakati yeye akiwa kwenye shughuli zake za
kila siku ambapo amesema fisi huyo alifika nyumbani kwao na kung’ata mtoto wake
baada ya mama yake kutoka nyumbani kwa muda mfupi.
“Kwa
kweli ni tukio la kusikitisha sana. Nilipata mshtuko mkubwa kuona mtoto wangu
amejeruhiwa vibaya kichwani na fisi. Hii si mara ya kwanza kwa matukio kama
haya kutokea hapa Nhelegani,” amesema Kapela.
Familia ya Kapela imeitaka serikali, kupitia mamlaka
za kudhibiti wanyama pori, kuhakikisha wanyama wakali kama fisi hawaonekani
tena katika maeneo ya makazi ya watu.
Kapela amesema kuwa katika eneo hilo tayari
yameripotiwa matukio manne ya wanyama hao kushambulia watu mwaka huu 2024.
“Matukio haya siyo ya mara ya
kwanza Nhelegani hapa yamekuwa
yakitokea, na kwa mwaka huu pekee tumeshuhudia matukio kama manne. Kwa kweli,
naomba mamlaka zinazohusika, hususan zile za wanyama pori, zichukue hatua.
Ikiwezekana, wawazuie au wapunguze idadi ya hawa wanyama kwa sababu wamekuwa
wengi mno na wanazagaa hovyo. Hata saa kumi jioni unaweza kukutana nao
wakitembea tu,”
amesema
Kapela.
“Naomba mamlaka za kuthibiti wanyama pori zipunguze au ziwaue kabisa
wanyama hawa, kama kuna uwezekano. Hali imekuwa ya wasiwasi sasa; mtu ukiwa
mbali na nyumbani, hasa ukiwaacha watoto, unakuwa na hofu kubwa,” ameongeza
Kapela.