Na Mapuli Kitina Misalaba
Mtoto mwenye umri wa miaka mitano wa familia ya
Shija Choyo, mkazi wa kitongoji cha Kalunde kijiji cha Nzoza kata ya Salawe,
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na
fisi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka matembezi na marafiki zake.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Nzoza Bwana
Hamis Masolwa amesema tukio hilo limetokea Desemba 26 wakati mtoto huyo na
wenzake walipokuwa wakirejea kutoka Senta ya Nzoza.
"Watoto
hao walikuwa zaidi ya kumi na wanne, wenye umri wa miaka nane na kuendelea,
lakini mtoto huyo alikuwa na miaka mitano tu. Fisi alitokea ghafla na kuanza
kuwafukuza. Watoto wakaanza kukimbia, lakini fisi alimfikia mtoto huyo na
kumshambulia," amesema Masolwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kelele za watoto ziliwafikia
wakazi wa eneo hilo, ambapo baba mmoja alifika eneo la tukio na kumkuta fisi
akimshambulia mtoto huyo. "Baba huyo alimbeba mtoto na kumpeleka nyumbani
kwa wazazi wake. Walipofanikiwa kupata usafiri wa kumpeleka hospitalini, tayari
mtoto alikuwa amefariki dunia," amesema Mwenyekiti huyo.
Mazishi ya mtoto huyo yalifanyika baada ya uchunguzi
wa daktari na ruhusa ya polisi na kwamba tukio hilo limetokea majira ya saa
kumi na mbili jioni, katika eneo lenye milima ambako fisi huyo alitokea.
Mwenyekiti Masolwa ametoa wito kwa wazazi na walezi
kuchukua tahadhari wakati wa sikukuu ya mwaka mpya, akiwataka kuhakikisha
watoto wanatembea na watu wazima ili kuepuka matukio kama hayo.
Katika mwezi huu wa Desemba, fisi huyo pia
ameripotiwa kumjeruhi mtoto mwingine katika kijiji cha Nzuzuli kata ya Mwenge,
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.