Na Mapuli Kitina Misalaba
Timu ya Mwasenge FC imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika Ligi ya Krismas
CUP wilayani Shinyanga Vijijini baada ya kuichapa Kano FC kwa mikwaju ya penati
4-2 ambapo mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kabla ya
kuamuliwa kwa penalti.
Akizungumza kuhusu mashindano hayo msimamizi wa
ligi, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, amesema fainali ya mashindano hayo
itafanyika Alhamisi, Desemba 19, 2024, katika Uwanja wa Mhangu, ambapo Salawe
FC itakutana na Beya FC.
“Siku
ya Alhamisi tutaendelea na mechi ya fainali, Sababu ya kuhamisha ratiba kutoka
Jumanne hadi Alhamisi ni msiba uliowakumba baadhi ya wachezaji wa Beya FC
ambapo Mazishi yatafanyika Jumatano, na kwa heshima hiyo, tumeamua kusogeza
mbele ratiba. Tunaomba radhi kwa mashabiki wote kwa mabadiliko haya ambayo
yamechangiwa na sababu zisizozuilika,” amesema Mwalimu
Kijida.
Ameongeza kuwa siku ya fainali kutakuwa na michezo
ya burudani kama kufukuza kuku, kuvuta kamba, ngoma za asili na wasanii
mbalimbali watapamba tukio hilo. “Wananchi wote wanakaribishwa kushuhudia mechi
na burudani hizo bila kiingilio,”.
Mashindano hayo yanadhaminiwa na Kampuni ya MCL, inayomilikiwa na Makamba Mussa Lameck, ambaye ni mfanyabiashara wa nafaka ambapo lengo la udhamini huo ni kuhamasisha na kukuza maendeleo ya michezo mkoani Shinyanga.