Na Mapuli Kitina Misalaba
Mashindano ya Ligi ya Makamba Lameck (Krismas CUP)
yameendelea kwa ushindani mkali kwenye uwanja wa Mhangu, kata ya Salawe, Wilaya
ya Shinyanga Vijijini, ambapo leo timu ya Mwasenge FC imeibuka na ushindi wa
magoli 2-0 dhidi ya Modern FC.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock
Kijida, amesema mechi ya leo imehitimisha hatua ya mzunguko wa kwanza katika
mashindano ya mtoano, huku akitoa ratiba ya mechi zijazo.
"Kwa
matokeo ya leo, Mwasenge FC wamefuzu kuingia hatua ya robo fainali na watakutana
na Mahando FC iliyoshinda mechi ya jana. Kesho, Jumamosi, tutaanza robo fainali
kwa mechi kati ya Kano FC na SEC Combine FC, huku Jumapili Beya FC ikichuana na
Mahakama . Siku ya Jumatatu tutapumzika kupisha maadhimisho ya siku ya
Uhuru," amesema Kijida.
Mgeni mwalikwa katika mechi hiyo, Afisa Mtendaji wa
kijiji cha Nzoza, Bi. Johari John, amewapongeza wachezaji kwa kujituma na
kuonyesha vipaji vyao.
"Michezo kama hii si burudani tu bali pia
huchangia afya, kujijenga kimwili, na kuwa fursa ya ajira kwa vijana.
Ninamshukuru Bwana Makamba Lameck kwa kuandaa mashindano haya na kuhamasisha
vijana kuonyesha uwezo wao," amesema Johari.
Kwa upande wake, Mtendaji wa kijiji cha Songambele,
Bi. Evalina Isack, amesisitiza umuhimu wa usalama katika mashindano hayo na
kutoa pongezi kwa mwandaaji.
"Tunashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi
kushiriki na kufanikisha mashindano haya. Tunaendelea kuhakikisha usalama wa
mali na watu wote waliopo hapa. Nampongeza Makamba Lameck kwa juhudi zake za
kuboresha maisha ya vijana kupitia michezo," amesema
Evalina.
Mashindano haya yanazidi kuonyesha umuhimu wa
michezo katika jamii, si tu kama burudani bali pia kama njia ya kujenga afya,
vipaji, na mshikamano. Krismas CUP inatarajiwa kufikia hatua ya fainali kabla
ya Sikukuu ya Krismasi.
Msimamizi wa ligi ya Krismas CUP, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, akizungumza.
Mgeni mwalikwa katika mechi hiyo, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nzoza, Bi. Johari John, akizungumza.
Mgeni mwalikwa katika mechi hiyo, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nzoza, Bi. Johari John, akizungumza.
Mtendaji wa kijiji cha Songambele, Bi. Evalina Isack, akizungumza.Mtendaji wa kijiji cha Songambele, Bi. Evalina Isack, akizungumza.