Na WMJJWM- Dar Es Salaam
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamisi amepongeza Mashirika ya Railway Children Africa, Citizen 4 Change na Small Things Tanzania kwa kushirikiana kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya uzoefu ya vijana ambao wamepata huduma ya Malezi Mbadala katika familia.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema hayo Desemba 12, 2024 Jijini Dar Es Salaam wakati wa halfa ya kupokea taarifa ya utafiti uliofanywa na Mashirika hayo.
“Ukweli usiopingika kwamba malezi ya familia ndio msingi imara wa malezi ya watoto pamoja na mchango mkubwa wa Makao ya Watoto; aidha utafiti wa kisayansi unaonesha kwamba yapo madhara yanayowapata watoto wakikaa kwa muda mrefu katika malezi ya kitaasisi hivyo utafiti uliofanyika ni muhimu kwani matokeo yake yatasaidia kutoa mwongozo wa namna ya kuimarisha malezi ya watoto katika ngazi ya familia” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Amesisitiza kwamba ni lazima Walezi wa Watoto katika Vituo vya Malezi Mbadala kuweka mpango wa huduma kwa Watoto na kuwaunganisha na familia zao au huduma zinazoakisi malezi ya mtoto katika ngazi ya familia kwa lengo la kuwawezesha watoto kuwa na maadili mema.
Aidha ametoa wito kwa wadau wa huduma za malezi mbadala kuendelea kushirikiana na kuunga mkono jitihada zinazofanywa Serikali hususani Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika kukamilisha tathmini hiyo kwa lengo la kuandaa mkakati wa kuimarisha Malezi ya Watoto katika ngazi ya familia.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Railway Children Africa Musa Mgata amesema Utafiti huo utasaidia kupata taswira kuhusu umuhimu wa Malezi mbadala kwa watoto ambao hawana wazazi au walezi ili kuweka mkazo kwa Serikali na wadau kuwekeza katika kuhamasisha Malezi mbadala kwa watoto hasa wanaoishi katika mazingira hatarishi hususan wale wanaofanya kazi na kuishi mitaani.