DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewahimiza wasajili wa Hati na Nyaraka Wasaidizi katika ofisi za Ardhi za Mikoa kuhakikisha wanatoa hati milki za ardhi kwa wakati kwa wananchi walioomba kupatiwa hati hizo.
Mhe Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Desemba 2024 wakati wa kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi yaliyoanza tarehe 2 Desemba 2024 jijini Dodoma.
"Wasajili wa Hati wanapataje afua kama mwananchi anasumbuliwa kupata hati milki ya ardhi kwa mwaka mmoja au miezi sita wakati angeweza kupata hati ndani ya wiki moja" amesema Mhe. Pinda.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wasajili wa Hati wakumbuke kuwa, wanapozuia ama kuchelewesha wananchi kupata hati kwa wakati watambue kuwa wanaikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.
"Kumekuwa na delay za hati kwa wanaoomba kumilikishwa ardhi nasisitiza hati zote zitoke bila kisingizio na ile njoo kesho ife"amesema.
Aidha, Mhe. Pinda amewapongeza watumishi wa sekta ya ardhi kwa kushiriki katika mageuzi makubwa ya wizara hiyo ambapo sasa wizara ya ardhi imeingia kwenye mfumo wa kidigitali (e-ardhi) jambo alilolieleza linalenga kuboresha huduma za sekta hiyo.
Ameongeza kuwa, ameridhishwa na utaratibu mzima wa kuwahudumia wananchi kupitia Klinik za Ardhi, utaratibu aliouelezea kuwa, umewafanya wananchi kuwa karibu na viongozi kwa kuwa wanafanikiwa kuwafikia tofauti na wanazifuata huduma ofisni.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaadhimisha Wiki ya Ardhi kuanzia tarehe 2 hadi 5 Desemba 2024 ambapo mbali mambo mengine wiki hiyo inatumika kujadili utoaji huduma za kisekta pamoja na uwepo mawasilisho mbalimbali kwa lengo la kufanya maboresho ya maeneo yenye changamoto.