Habari zilizotufikia muda huu zinaeleza kuwa wabunge zaidi ya 50 waliokuwa wakisafiri kwa basi kutoka Dodoma kwenda Nchini Kenya kushiriki michezo wamepata ajali eneo la Mbande mkoani Dodoma.
Wabunge kadhaa wamepata majeraha ya Mwili kutokana na ajali hiyo .
Imeelezwa kuwa basi hilo la Bunge likiwa katika mwendo wa kawaida lilikutana na changamoto ya gari jingine lililokuwa limeangusha mizigo barabarani na wakati dereva akijaribu kukwepa mizigo hiyo ndipo basi hilo lilipoacha njia na kuingia Porini.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa miongoni mwa wabunge waliojeruhiwa ni pamoja na mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga ,Mbunge wa Iringa mjini Jesca Msambatavangu,mbunge wa Viti maalum chadema Grace Tendega
Shuhuda huyo alisema basi lililopata ajali ni moja kati ya mabasi manne ya Shabiby yaliyokuwa yanawasafisha kwenda kwenye mashindano ya mabunge ya Afrika Mashariki Mombasa Kenya, amesema kuwa ajali hiyo imetokea leo alfajiri baada ya basi moja kudaiwa kugonga nyuma ya lori lililokuwa limesimama katika Barabara hiyo ya Morogoro - Dodoma.
"Tunashukuru Mungu wenzetu wamenusurika basi moja kati ya manne tuliyokuwa tunasafiria limepata ajali na baadhi ya wenzetu wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali za Uhuru na Benjamini Mkapa kwa ajili ya matibabu, hatujui hadi sasa wenzetu wanaendeleaje, nasi bado tupo eneo la ajali," amesema Mbunge huyo ambae hakutaka jina lake kuandikwa kwa kuwa si Msemaji wa bunge
Msafara huo ambao ulitakiwa kupitia Chalinze na Tanga kwenda Mombasa, umejumuisha wabunge na watumishi wa Bunge zaidi ya 120 wanaokwenda kushiriki michezo mbalimbali inayotarajia kuanza kesho Desemba 7 hadi Desemba 17 mwaka huu na kushirikisha timu za mabunge ya Nchi 7 likiwemo Bunge la Afrika Mashariki.
Tunaedelea kumtafuta Msemaji wa bunge ili kupata undani wa tukio hili tutawajuza zaidi pamoja na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi, DCP, David Misime
TAARIFA YA BUNGE
Moja ya basi lililokuwa limewabeba Waheshimiwa Wabunge wanaoelekea kwenye Mashindano ya Michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki limepata ajali ya kugongana na lori la mizigo maeneo ya Mbande Kongwa asubuhi hii.
Majeruhi wa ajali hiyo wamekimbizwa Hospitali ya Uhuru na Hospitali ya Benjamini Mkapa za Mkoani Dodoma